Tuesday, October 2, 2012

SUGU ADATA BAADA YA KUPATA MTOTO

UMESHAWAHI kuona mtu mzima amedata? Basi kwa taarifa yako habari za kupata mtoto, zilipomfikia Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, alitulia kama maji mtungini kwa muda, baada ya muda mfupi akaamka na kushangilia kwa nguvu, Showbiz inakumegea.
Kwa watu waliomzoea Sugu, walishangazwa na furaha yake, kwani ‘mudi’ yake ilikuwa juu mno baada ya kusoma SMS ya kumueleza kwamba yeye ni baba wa mtoto wa kike. Waliokuwa karibu yake, walipomuuliza, Sugu alitamka mfululizo: “My daughter, I’m now a father. My daughter, I’m the happiest MP right now.”
Alimaanisha: Binti yangu, sasa mimi ni baba. Binti yangu, sasa mimi ni mbunge mwenye furaha zaidi.
Jumatano iliyopita (Septemba 26, 2012) usiku, Sugu alipokea SMS kutoka kwa mzazi mwenzake, anayekwenda kwa jina la Faiza, asubuhi ya siku iliyofuata, hakuweza kuendelea kukaa Mbeya, alisafiri kwa mkoko wake wa heshima, Toyota Land Cruiser Amazon hadi Dar kumuona binti yake.
Mtoto huyo, Sugu amempa jina la Sasha-Desderia Joseph Mbilinyi. Kama ulikuwa hujafunuliwa, jina la Desderia ni la mama mzazi wa mbunge huyo, anayeitwa Desderia Mbilinyi ‘Mama Mbilinyi’.
Akizungumza na Showbiz, Sugu alisema: “Kwanza namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kumpata Sasha-Desderia. Ni mtoto ambaye amekuja ndani ya mahitaji yangu. Yaani nilimhitaji na kweli amekuja.
“Kwa mama wa mtoto (Faiza), namuomba sana Mungu atujaalie maisha marefu yenye furaha na maelewano, tuweze kumlea mtoto wetu.”
Sasha-Desderia, ni mtoto wa kwanza wa Sugu ambaye mbali na ubunge, jina lake lipo juu kwa takriban miongo miwili sasa kutokana na harakati zake kwenye muziki wa Hip Hop na Bongo Fleva, akiwa ameshatoa albamu 10, pamoja nyimbo zinazobamba zaidi ya 40.

No comments:

Post a Comment