Joseph Shamba 'Vengu'.
TABIA za wasanii wa Kundi la Orijino Komedi ni tatizo kubwa. Unaweza
kujiuliza kwa nini sasa hivi wasanii hao wamepoteza mvuto kwenye jamii.
Mtindo wa maisha yao hauna mvuto.
Endapo mtindo wa maisha yako
utakuwa unawafurahisha watu, utaendelea kupendwa. Ikitokea unawaudhi
watu, mvuto wako lazima utapotea. Komedi wajiangalie leo, kwa nini
hawana mvuto?
Wajipime walivyokuwa mwaka 2007 hadi mwaka 2009, waone
namna walivyoishika nchi. Baada ya hapo wajiangalie walivyogeuka wa
kawaida kuanzia mwaka 2009 mpaka sasa.
Huwezi kuwakera watu halafu
wakaendelea kukupenda. Asili yetu Watanzania ni kuwakumbatia watu wema.
Inawezekanaje watu wabaguzi, wanaowanyanyapaa wengine, wakakubalika
kwenye jamii yetu?
Ni jambo lisilowezekana. Ndiyo maana Orijino
Komedi leo hii hawana mvuto. Dhambi ya kumbagua Vengu (Joseph Shamba),
kumfanya aishi kama mtwana wao wakati ni mwenzao, haiwezi kuwaacha
salama.
Dhambi ya kuwadhihaki watu ambao uchumi wao siyo mzuri,
wakiwasema eti wamefulia, wakati nao bado ni wasafiri kwenye haya
maisha, haiwezi kuwaacha salama. Kuna matokeo lazima yawakute.
Ni
lazima walipe gharama za vitendo vyao viovu. Gharama hizo ndiyo matokeo
ya sasa tunayoyaona. Namba ya watazamaji wa vipindi vya Orijino Komedi,
imeshuka kwa kiasi kikubwa mno.
Siyo siri, kipindi cha nyuma Komedi
ilikuwa ndiyo habari ya mjini. Kila Alhamisi jioni ilikuwa ni hekaheka
kwenye runinga. Baa zilifurika, vibanda vya video show (vibanda umiza)
vilijaa kupita kiasi. Waliteka jamii kisawasawa.
Kuna wakati Komedi
ilirejesha amani ya nyumba, kwani baba na mama, walijumuika pamoja na
watoto kila Alhamisi jioni, sebuleni kutazama vichekesho vya vijana hao.
Watu
hao wamewakimbia. Ni matokeo ya tabia ambazo si njema walizozionesha.
Ni malipo yao baada ya kubweteka kwa kudhani wameshafika kwenye kilele
cha maisha. Hadhi yao imeshuka mno.
Zamani Komedi ilikuwa programu
inayowalazimisha watu kutenga muda wa kutazama vichekesho vyao. Hivi
sasa, wenye kiu ya kutazama ni watoto na kwa watu wazima, ni wale
waliokuta runinga imewekwa TBC1, wakaona wapoteze muda huku wakijiuliza:
“Hivi hawa kumbe bado wapo?”
Kama msemo wao wenyewe, ni wazi Orijino
Komedi wamefulia. Hata idadi ya matangazo waliyokuwa wanapata zamani
hivi sasa hawana. Hii iwape sababu ya kujipima, waangalie makosa yao, la
sivyo watapotea kabisa.
Ni vijana wenye vipaji, kwa hiyo ni vizuri
wakatetea ajira zao. Wabadilike leo. Waache kubweteka, wao bado ni
wachanga mno. Maisha ni safari ndefu, naamini wakijirudi, jamii
itawapenda tena.
Hivi hawajiulizi leo Ze Comedy ya akina Bambo
(Dickson Makwaya), inavyoteka soko la vichekesho nchini kupitia Channel 5
(EATV)? Unapoona akina Mtanga wanageuka habari ya mjini, maana yake
Joti na Mpoki, kwisha habari yao.
Kushuka kwa akina Joti, inawezekana
ikawa ni matokeo pia ya jeuri yao waliyomuonesha mzee Reginald Mengi
wakati ndiye aliyewafanya wakaonekana hapa nchini.
Nawashauri
wajirudi, watubu mateso waliyomsababishia Vengu mpaka wakamfanya awe
chapombe. Mbaya zaidi, hata walipoambiwa kwamba msanii huyo ana hali
mbaya, wapo waliojibu, “atajijua.”
Kijana wa watu anateseka,
amenyang’anywa gari, ikadaiwa hata fedha zake nyingi zimefichwa kwenye
akaunti ya mmoja wa wasanii wa kundi hilo (jina ninalo na habari hiyo
iliandikwa gazetini). Mateso hayo ya moyo, yakamfanya ajiliwaze kwa
pombe.
Huko kwenye pombe, akawa anazitwika mpaka anakuwa ‘tilalila’.
Anapoteza fahamu, sisi Global Publishers, tunawapigia simu wasanii
wenzake, wajitokeze kumpa msaada, msanii mmoja (jina ninalo), akajibu:
“Huyo atajijua yeye mwenyewe.”
Ni mateso yaliyoje kuishi kwenye jamii
ya watu ambao hawakupendi? Hayo ndiyo maumivu makubwa aliyoishi nayo
Vengu. Hii ikamfanya awe rafiki mkubwa wa pombe ili ajiliwaze kwa
machungu ya kubaguliwa na wenzake.
Kwa hakika, jumlisha mateso ya
kubaguliwa na wenzake, jumlisha na maradhi yaliyomchukua kwa muda sasa,
ni wazi msanii huyo hajawahi kufurahia maisha ya kundi hilo kama ilivyo
kwa wenzake.
Itaendelea kesho kwenye Gazeti la Amani.