Wema.
Diamond.
Hoteli ya Giraffe walimolala Diamond na Wema.
Gari la Wema likiwa eneo la hoteli ya Giraffe.
Gari la Diamond likiwa nje ya hoteli hiyo.
Musa Mateja na Imelda Mtema
NDIVYO ilivyokuwa, staa mkali wa filamu Bongo, Wema Sepetu na
mwanamuziki wa Bongo Fleva ambaye kwa sasa yupo juu, Nasibu Abdul a.k.a
Diamond ‘Plantinum’ wamenaswa katika hoteli yenye hadhi ya nyota tano
Giraffe iliyopo Mbezi, jijini Dar es Salaam.
MESEJI YA KWANZA KWENYE SIMU YA PAPARAZI
Asubuhi ya Juni 26,
2012, ujumbe mfupi wa maneno (sms) uliingia kwenye simu ya paparazi wetu
ukidondosha madai mazito kuwa, mastaa hao waliowahi kuwa wachumba na
baadaye kumwagana kinomanoma, wako kwenye hoteli hiyo ‘wakiponda raha
kwani kufa kwaja’.
Meseji hiyo ikafafanua: “Tena wapo toka jana,
Wema yeye yupo toka alipomaliza ile shughuli yake na Omotola yule mdada
wa Naijeria (Nigeria).”
MAPAPARAZI WAINGIA MZIGONI
Baada ya kupata ujumbe huo, waandishi
wetu walikaa kama kamati mbele ya mhariri wao, wakaandaa zana
mbalimbali zikiwemo kamera na vifaa vya kurekodia kwa ajili ya
kufuatilia ukweli wa meseji hiyo.
GARI LA DIAMOND NJE YA HOTELI
Waandishi wetu walifika hotelini
hapo saa 3:46 ambapo nje ya hoteli hiyo, mapaparazi hao walianza kuamini
Platinum yupo ndani baada ya kuliona gari lake aina ya Toyota Prado,
lakini katika kuzungusha makengeza yao hawakuweza kulitia machoni gari
la Wema.
MBELE YA MAPOKEZI YA HOTELI
Mbele ya kaunta ya mapokezi, waandishi waliomba kuonana na Wema Sepetu.
Mtu wa Mapokezi: Nimwambie nani?
Musa: Mwambie baby wake.
Mtu wa Mapokezi: Baby wake yupi?
Musa: Musa Mateja.
Mtu wa Mapokezi alimtwangia simu Wema ambapo alipoambiwa ni Musa Mateja
aliamuru asubiri eneo hilo mpaka atakapoitwa kwenda chumbani.
DIAMOND HUYO!
Waandishi wakiwa wamepiga kambi wakisubiri kuitwa,
ghafla Diamond alishuka akiwa mbiombio kuelekea kwenye gari lake kama
mtu anayewahi. Mapaparazi wetu walimfuata hadi kwenye gari ambapo
alikuwa ameshaingia.
MSIKIE ALICHOSEMA
Bila kupoteza muda alisomewa mashitaka yake ‘eituzedi’ ambapo alivuta pumzi kwa nguvu kisha akafunguka:
“Mimi hata sijui kama Wema yupo hapa hotelini, kwani yupo hapa? Chumba
namba ngapi? Mimi nilikuja kwenye mambo yangu, kwa sasa natunga mashairi
ya wimbo mwingine kwa hiyo nilikuja tangu jana ili kufanya kazi yangu
kwa ufanisi, unajua napenda kuwa sehemu yenye utulivu mkubwa.
“Unajua nini, nilikuwa Morogoro, nimerudi jana, nikaja hapa kumfuata
Jeff, si unajua yule mshikaji wangu sana? Kuna wakati pia huwa nakuja
pale kwenye hoteli moja ipo jirani na ofisini zenu, pale napo pazuri
sana, nimewahi kulala. Ha! Ha! Ha! Musa bwana!”
MENEJA WA WEMA
Meneja wa Wema, Martin Kadinda naye alikutana na waandishi wetu ambapo alishtuka kumwona Diamond kwenye gari lake.
Martin: Khaa! Diamond unaweza kuja hapa hotelini halafu unaondoka usinitafute wakati unajua mimi nipo na tuna ishu yetu?
Diamond: (kicheko tu).
WAANDISHI WARUDI MAPOKEZI, WAITWA KWA WEMA
Baada ya kumalizana na
Diamond waandishi wetu walirudi mapokezi ambapo walipelekwa kwenye
chumba alichomo supastaa mwenye chemchemi za skendo Bongo, Wema na
kumkuta akiwa na rafiki yake kipenzi (lakini asiyekubalika na mama
yake), Snura Mushi.
Wema, baada ya kusomewa mashitaka yake alishtuka sana na kuonesha mshangao kusikia Diamond alilala hotelini hapo.
Alisema kuwa yeye ndiyo kwanza yuko kitandani na alikuwa amelala na
Snura, habari ya Diamond kuwepo hotelini hapo anasikia kutoka kwa
mapaparazi lakini yeye hajui chochote.
“Jamani mnavyoniona mimi hapa
ndiyo kwanza nimeamka, hata nje sijatoka na watu wa kwanza kuongea nao
ni nyinyi, mimi sijui kabisa kama huyo mtu yuko hapa. Kwanza alifuata
nini hapa jamani?”
Amani: Sisi tulivyosikia alikuwa na wewe, sasa wewe tena unatuuliza sisi, tutajua vipi? Si ndiyo maana tumekuja?
Wema: Jamani kusema kweli… (akachukua simu na kumpigia mwanaume
aliyedai ni mpenzi wake) dady, wamekuja waandishi hapa wanasema
wamesikia nimelala na Diamond, we si tumeongea hadi usiku sana?
MASWALI MAGUMU
Inawezekana Diamond akafika hotelini hapo bila Wema kuwa na taarifa?
Ni kweli kwamba, Wema aliweka kambi pale kwa lengo la kujipumzisha tu akiwa na shoga yake Snura?
Utulivu anaodai Diamond aliufuata pale hotelini ulikosekana sehemu nyingine yoyote (hasa nyumbani) ikiwemo ufukweni?
Kwa nini Wema aliharakisha kumpigia simu huyo aliyemuita mpenzi wake
kumwambia kuhusu waandishi kufuatilia habari ya kulala na Diamond wakati
akidai walizungumza hadi usiku sana?
UKWELI UPO KWA WEMA, DIAMOND
Kwa maelezo yao hayo, bado ukweli
unabaki kuwa siri yao. Hata hivyo, penzi halina siri, kama wanaficha,
mapaparazi wapo macho kuwafuatilia na kama ni kweli wanatoka, siku moja
mambo yatakuwa hadharani.