Monday, June 18, 2012
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: ikulumawasiliano@yahoo.com
Fax: 255-22-2113425 |
![]() |
PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120,
DAR
ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametuma
salamu za rambirambi kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,
Mheshimiwa Fenella Mukangara kuomboleza kifo cha Mhariri Mtendaji wa Gazeti la
JamboLeo, Ndugu Willy Edward Ogunde kilitokea usiku wa kuamkia jana, Jumapili,
Juni 17, 2012 mjini Morogoro.
Katika salamu
zake za rambirambi, Mheshimiwa Rais Kikwete amesema kuwa ameshtushwa na
kusikitishwa na kifo cha ghafla cha Ndugu Willy Edward Ogunde ambaye amepoteza
maisha akiwa bado kijana ingawa tayari alikuwa amekwishakutoa mchango mkubwa katika
maendeleo ya tasnia ya habari kutokana na umakini wake, uzingatiaji wa weledi kikamilifu na misingi mingine mikuu
ya uandishi wa habari.
“Nimepokea kwa
mshtuko mkubwa na huzuni nyingi kifo cha ghafla cha Ndugu Willy Edward Ogunde
ambaye nimejulishwa kuwa kilitokea usiku wa kuamkia jana, Jumapili, huko
Morogoro ambako alikuwa amekwenda kikazi. Ndugu Willy Edward Ogunde amepoteza
maisha akiwa bado kijana sana hata kama ni kweli katika muda mfupi wa maisha
ametokea kuwa mfano wa kuigwa katika tasnia ya habari kwa mchango wake wa
kudumisha weledi na misingi mingine mikuu ya uandishi wa habari.”
Ameongeza Rais
Kikwete: “Nakutumia wewe Mheshimiwa Waziri salamu za dhati ya moyo wangu za
rambirambi kuomboleza kifo cha kijana huyu wetu na mwanataaluma wako. Aidha,
kupitia kwako nakuomba uniwasilishie salamu zangu kwa wanataaluma wote wa
tasnia ya habari nchini kwa kuondokewa na mwenzao. Lakini zaidi, nakuomba
unifikishe salamu zangu nyingi kwa wanafamilia, ndugu na jamaa wa Marehemu
Willy Edward Ogunde.”
“Wajulishe
kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa kwa sababu msiba wao ni msiba wangu pia.
Naelewa machungu yao katika kipindi hiki kigumu cha kufiwa na mpendwa wao.
Nawaombea subira na uvulivu. Aidha, wajulishe kuwa naungana nao katika kumwomba
Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke pema peponi roho ya Marehemu Will
Edward Ogunde. Amina,” amesisitiza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
IMETOLEWA
NA:
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
18
Juni, 2012
DAR
ES SALAAM
No comments:
Post a Comment