Gari la Wolper aina ya BMW X6.
Jacqueline Masawe ‘Wolper’.
Na Gladness Mallya
SAKATA la kukamatwa kwa lile gari la kifahari aina ya BMW X6 lenye
thamani ya takriban Sh. milioni 175 la staa wa filamu za Kibongo,
Jacqueline Wolper Masawe limeibua kisanga kipya, Ijumaa lina kila kitu
mkononi.HABARI BILA WASIWASI
Habari bila wasiwasi zimeeleza kuwa
pedeshee maarufu jijini Dar es Salaam, Mohamed Ndama a.k.a Ndama Mtoto
wa Ng’ombe ndiye aliyemwingiza Wolper mkenge hivyo jamaa huyo ametiwa
mbaroni akidaiwa kuhusika kuliingiza Bongo kinyemela.
Kwa mujibu wa
chanzo kisichokoroma ambacho ni rafiki mkubwa wa Wolper, Ndama aliwekwa
nyuma ya nondo katika Kituo cha Kati (Central), Dar Jumanne wiki hii
baada kutajwa kuwa alihusika na uingizaji wa gari hilo hapa nchini.
Chanzo hicho kiliendelea kutiririka kuwa mchumba wa Wolper, Abdalla
Mtoro ‘Dallas’ au Rais wa Ununio alitoa fedha kwa pedeshee huyo na
kumtaka atafute gari la kifahari kwa ajili ya mchumba’ke (Wolper).
GARI LENYE HADHI YA WOLPER
Kilidai kuwa katika kutafuta gari
lenye hadhi ya Wolper ndipo akampatia mwigizaji huyo lile BMW X6 na
kubandikwa namba za usajili T 574 BXF.
TURUDI NYUMA KIDOGO
Katika habari ya kukamatwa kwa gari hilo na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliyoripotiwa kwa mara ya kwanza na
gazeti pacha la hili, Ijumaa Wikienda, ilielezwa kuwa lilikamatwa kwa
sababu liliingizwa nchini bila vibali husika na pia kudaiwa ushuru
unaokadiriwa kufikia Sh. milioni 70.
TUENDELEE NA CHANZO
“Unajua Ndama aliwapiga changa la macho Wolper na Dallas kwa sababu alipewa madaraka yote ya kutafuta gari hilo la kifahari.
“Ilikuwa ni vigumu kwa Wolper kutia shaka kwa sababu alipokabidhiwa
lilikuwa na ‘dokumenti’ zote na ndiyo maana akawa anatanua nalo bila
wasiwasi, lakini ndo hivyo ngoja tuone itakuwaje,” kilisema chanzo chetu
cha kuaminika na kuongeza:
“Jumanne ndiyo aliitwa Central akahojiwa kwa saa kadhaa na Wolper akiwepo.
“Baada ya mahojiano pale kituoni hadi jioni ndipo akatupwa ‘lokapu’.
“Sijui kama alitoka kwa dhamana au alilala pale kituoni, fuatilieni.”
Baada ya kumwagiwa data, Ijumaa liliingia mzigoni ndipo likafanikiwa
kupata ukweli kuwa Ndama alifunguliwa jalada la kesi namba
CD/RB/7005/2012 na CD/IR/2624/2012.
KOVA ANASEMAJE?
Jumatano wiki hii, Ijumaa lilifunga safari hadi
ofisini kwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman
Kova ili kulizungumzia tukio hilo lakini jitihada ziligonga mwamba baada
ya kumsubiri muda mrefu kwa maelezo kwamba alikuwa kwenye kikao nyeti.
WOLPER ANAKATAKATA
Alipotafutwa Wolper alikuwa akikatakata simu kila alipopigiwa kwenye kilongalonga chake cha kiganjani.
TUMEFIKAJE HAPA?
Gari la Wolper lilikamatwa Juni 28, mwaka huu na
kampuni ya Mnada ya Majembe kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo
kuingizwa nchini kinyemela na kutolipiwa ushuru kwa muda wa miaka 5.