Friday, July 20, 2012

DOTNATA ABADILI DINI





Husna Posh ‘Dotnata’.
Hamida Hassan na Gladness Mallya
MSANII mkongwe katika tasnia ya filamu za Kibongo, Husna Posh ‘Dotnata’ amebadili dini kutoka Uislam na kuwa Mkristo kwa kile alichodai ni kutengeneza maisha yake baada ya kuhangaika na mambo ya dunia kwa muda mrefu.
Akichezesha taya na Ijumaa, Dotnata alisema amefikia uamuzi huo baada ya kuugua na kuhangaika kwa waganga wengi kwa muda mrefu bila ya mafanikio.
Dotnata ametaja sababu nyingine ni mama yake mzazi ambaye alifikia hatua ya kususa kumtembelea nyumbani kwake hasa kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani akimtaka aokoke.
“Mama alinipa masharti kwamba nitakapookoka ndipo atakapofika kwangu jambo ambalo lilikuwa linaninyima amani na kunifanya nichukue uamuzi huo,” alisema.
Dotnata ambaye awali alikuwa ni Mkristo amebatizwa upya na anatumia jina lake la awali kabla ya kuwa Muislam la Iluminata na amejiunga na Kanisa la Ufufuo na Uzima (kwa Gwajima) lililopo Kawe jijini Dar.
“Nitakuwa nahudhuria kanisani siku tatu kwa wiki kwa ajili ya kujifunza neno, pia nyumbani kwangu nimetenga sehemu maalum kwa ajili ya kuangalia mahubiri ya mtumishi wa Nigeria TB Joshua kwa njia ya runinga,” alisema.
Dotnata amesema kuwa ameapa kutogeuka tena kwani ataendelea na wokovu wake mpaka dakika ya mwisho wa maisha yake ili atakapozikwa ndugu na jamaa zake wacheze sebene la Yesu.
“Naomba niliowakosea wanisamehe kwani wengine nimeshawapigia simu na kuwaomba radhi, hivyo natumia fursa hii kuwaomba wengine wote wanisamehe kwa sababu nimeanza maisha mapya,” alisema Dotnata.
Alipoulizwa kuwa mumewe Posh amelipokea vipi suala la kuokoka kwake, Dotnata alisema mumewe hana matatizo na anaona ni jambo la kawaida na maisha ya upendo na amani yanaendelea kutawala ndani ya ndoa yao.

No comments:

Post a Comment