Wednesday, August 29, 2012

Assad ahitaji muda zaidi kushinda vita

 29 Agosti, 2012 - Saa 10:32 GMT
Rais Bashr Al Assad
Rais wa Syria Bashar al-Assad amesema kuwa serikali yake inahitaji muda wa ziada kuweza kushinda vita dhidi ya waasi nchini humo.
Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni kinachounga mkono serikali ya Assad,
rais huyo pia alipuuza tamko kuwa haiwezekani kutenga maeneo ya kutolea misaada katika maeneo ya mipaka nchini humo,
Wanaharakati wa upinzani wanadai kuwa jeshi limefanya mashambulizi katika maeneo mengi ya nchi hiyo kutaka kudhibiti maeneo yaliyotekwa na waasi.
Mapambano makali yaliripotiwa kutokea siku ya Jumanne katika mji mkuu Damascus, Aleppo na mkoa wa kaskazini masharibi wa Idlib.
Bwana Assad amesema kuwa serikali yake iko kwenye vita ndani na nje ya nchi.
"bila shaka tunahitaji muda zaidi kuweza kumaliza vita hivi katika njia inayofaa. Lakini ninachoweza kusema ka neno moja tu ni tunapiga hatua''. Bwana Assad alisema.
"hali kwa sasa angalau ni nzuri, lakini bado hatujafika mwisho. Hilo bila shaka linahitaji muda zaidi'' alisema Assad
''Maafisa wa ulinzi wanafanya kitendo ha ushujaa kwa kila hali. Lakini waasi hawataruhusiwa kueleza hofu wala hawataruhusiwa kiufanya hivyo.'' aliongeza rais Assad.
Kila mtu hapa nchini ana wasiwasi kuhusu hali ya nchi yetu, hilo ni jambo la kawaida.Ninawaambia wananchi wa Syria, mustakabali a nchi hii uko mikononi mwenu, wala sio mikononi mwa watu wengine''.
Rais aliwakejeli maafisa wakuu wa serikali na jeshi ambao wameasi serikali katika miezi ya hivi karibuni akisema kuwa hatua hiyo iliweza kuisafi serikali mwanzo na kisha nchi kwa ujumla.

MATESO YA VENGU, CHANZO NI ORIJINO KOMEDI WENYEWE - 3

Joseph Shamba 'Vengu'.
TABIA za wasanii wa Kundi la Orijino Komedi ni tatizo kubwa. Unaweza kujiuliza kwa nini sasa hivi wasanii hao wamepoteza mvuto kwenye jamii. Mtindo wa maisha yao hauna mvuto.
Endapo mtindo wa maisha yako utakuwa unawafurahisha watu, utaendelea kupendwa. Ikitokea unawaudhi watu, mvuto wako lazima utapotea. Komedi wajiangalie leo, kwa nini hawana mvuto?
Wajipime walivyokuwa mwaka 2007 hadi mwaka 2009, waone namna walivyoishika nchi. Baada ya hapo wajiangalie walivyogeuka wa kawaida kuanzia mwaka 2009 mpaka sasa.
Huwezi kuwakera watu halafu wakaendelea kukupenda. Asili yetu Watanzania ni kuwakumbatia watu wema. Inawezekanaje watu wabaguzi, wanaowanyanyapaa wengine, wakakubalika kwenye jamii yetu?
Ni jambo lisilowezekana. Ndiyo maana Orijino Komedi leo hii hawana mvuto. Dhambi ya kumbagua Vengu (Joseph Shamba), kumfanya aishi kama mtwana wao wakati ni mwenzao, haiwezi kuwaacha salama.
Dhambi ya kuwadhihaki watu ambao uchumi wao siyo mzuri, wakiwasema eti wamefulia, wakati nao bado ni wasafiri kwenye haya maisha, haiwezi kuwaacha salama. Kuna matokeo lazima yawakute.
Ni lazima walipe gharama za vitendo vyao viovu. Gharama hizo ndiyo matokeo ya sasa tunayoyaona. Namba ya watazamaji wa vipindi vya Orijino Komedi, imeshuka kwa kiasi kikubwa mno.
Siyo siri, kipindi cha nyuma Komedi ilikuwa ndiyo habari ya mjini. Kila Alhamisi jioni ilikuwa ni hekaheka kwenye runinga. Baa zilifurika, vibanda vya video show (vibanda umiza) vilijaa kupita kiasi. Waliteka jamii kisawasawa.
Kuna wakati Komedi ilirejesha amani ya nyumba, kwani baba na mama, walijumuika pamoja na watoto kila Alhamisi jioni, sebuleni kutazama vichekesho vya vijana hao.
Watu hao wamewakimbia. Ni matokeo ya tabia ambazo si njema walizozionesha. Ni malipo yao baada ya kubweteka kwa kudhani wameshafika kwenye kilele cha maisha. Hadhi yao imeshuka mno.
Zamani Komedi ilikuwa programu inayowalazimisha watu kutenga muda wa kutazama vichekesho vyao. Hivi sasa, wenye kiu ya kutazama ni watoto na kwa watu wazima, ni wale waliokuta runinga imewekwa TBC1, wakaona wapoteze muda huku wakijiuliza: “Hivi hawa kumbe bado wapo?”
Kama msemo wao wenyewe, ni wazi Orijino Komedi wamefulia. Hata idadi ya matangazo waliyokuwa wanapata zamani hivi sasa hawana. Hii iwape sababu ya kujipima, waangalie makosa yao, la sivyo watapotea kabisa.
Ni vijana wenye vipaji, kwa hiyo ni vizuri wakatetea ajira zao. Wabadilike leo. Waache kubweteka, wao bado ni wachanga mno. Maisha ni safari ndefu, naamini wakijirudi, jamii itawapenda tena.
Hivi hawajiulizi leo Ze Comedy ya akina Bambo (Dickson Makwaya), inavyoteka soko la vichekesho nchini kupitia Channel 5 (EATV)? Unapoona akina Mtanga wanageuka habari ya mjini, maana yake Joti na Mpoki, kwisha habari yao.
Kushuka kwa akina Joti, inawezekana ikawa ni matokeo pia ya jeuri yao waliyomuonesha mzee Reginald Mengi wakati ndiye aliyewafanya wakaonekana hapa nchini.
Nawashauri wajirudi, watubu mateso waliyomsababishia Vengu mpaka wakamfanya awe chapombe. Mbaya zaidi, hata walipoambiwa kwamba msanii huyo ana hali mbaya, wapo waliojibu, “atajijua.”
Kijana wa watu anateseka, amenyang’anywa gari, ikadaiwa hata fedha zake nyingi zimefichwa kwenye akaunti ya mmoja wa wasanii wa kundi hilo (jina ninalo na habari hiyo iliandikwa gazetini). Mateso hayo ya moyo, yakamfanya ajiliwaze kwa pombe.
Huko kwenye pombe, akawa anazitwika mpaka anakuwa ‘tilalila’. Anapoteza fahamu, sisi Global Publishers, tunawapigia simu wasanii wenzake, wajitokeze kumpa msaada, msanii mmoja (jina ninalo), akajibu: “Huyo atajijua yeye mwenyewe.”
Ni mateso yaliyoje kuishi kwenye jamii ya watu ambao hawakupendi? Hayo ndiyo maumivu makubwa aliyoishi nayo Vengu. Hii ikamfanya awe rafiki mkubwa wa pombe ili ajiliwaze kwa machungu ya kubaguliwa na wenzake.
Kwa hakika, jumlisha mateso ya kubaguliwa na wenzake, jumlisha na maradhi yaliyomchukua kwa muda sasa, ni wazi msanii huyo hajawahi kufurahia maisha ya kundi hilo kama ilivyo kwa wenzake.
Itaendelea kesho kwenye Gazeti la Amani. 

SPIKA ANUSURIKA RISASI, MABOMU YA POLISI YALIYOLENGWA CHADEMA

Spika wa Bunge la Jamhuri  ya Muungano ya Tanzania, Anna Makinda.
Moshi ukiwa umetanda wakati wa vurugu za kuzuia maandamano ya Chadema.
SPIKA wa Bunge la Jamhuri  ya Muungano ya Tanzania, Anna Makinda,  juzi Jumatatu msafara wake ulinusurika risasi na mabomu ya machozi ya polisi wa Morogoro waliyokuwa wameyalenga kwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) eneo la Msamvu, barabara kuu ya Morogoro-Dar es Salaam. Mwandishi wetu alimshuhudia spika akitokea lringa kwa gari na kupita eneo la Msamvu ambapo muda mfupi baadaye polisi walianza kurusha mabomu ya machozi na risasi na kumwua kijana Ally Zolla  na vijana wengine wawili kujeruhiwa.
(NA DUNSTAN SHEKIDELE / GPL, MOROGORO)

Friday, August 24, 2012

WASANII NYOTA WA BONGO MOVIE WAVAMIA MJI WA MOSHI, WAKIRI WAZI TAMASHA LASERENGETI FIESTA LEO PATAKUWA HAPATOSHI CHUO CHA USHIRIKA

Friday, August 24, 2012

Mmoja wa wasanii mahiri katika fani ya uigizaji hapa nchini, Wema Sepetu akifanya mahojiano mafupi na Millard Ayo wa Clouds FM mapema leo kwenye amsha amsha ya tamasha la Serengeti Fiesta ambalo linafanyika jioni ya leo mpaka lyamba ndani ya uwanja wa chuo cha Ushirika, ndani ya mji wa Moshi,ambapo katika tamasha hilo kiingilio kimepangwa kuwa ni nusu mnyama tu a.k.a 5,000/= kwa kila kichwa. Wema Sepetu pia aalisema ujio wao ndani ya mji wa Moshi,kuwa wao kama Wasanii Nyota wa Filamu wamewasili mkoani humo kusaka vipaji vipya mbalimbali vya filamu,usahili huo unafanyika kwenye ukumbi wa Mr Price,ulioko mtaa wa Malindi.
Mtangazaji wa Clouds FM,Millard Ayo akiwa Live mapema leo mtaa wa Malindi katika mpango mzima wa amsha amsha kwa wakazi wa Moshi kuhusiana na tamasha la Serengeti Fiesta 2012,ambapo pia katika tamasha hilo kutatolewa zawadi mbalimbali ikiwemo gari ndogo aina ya Vits kama uinavyo pichani ikinadiwa vilivyo.
Kawa kawa amsha amsha ya tamasha la Serengeti Fiesta pia linatoa mafuta kwa magari daladala,pikipiki sambamba na baji lita 10 ama tano kutoka kampuni ya Gapco ambao pia ni sehemu ya wadhamini wa tamasha hilo.
Msanii mwingine nyota katika tasnia ya filamu,Aunt Ezekiel akielezea ni namna tamasha la Serengeti Fiesta lilivyowambamba wakazi wa mji wa Moshi na vitongoji vyake,na pia ujio wao kuwatafuta wasanii wapya chipukizi katika tasnia hiyo ambayo imekuwa ikikua siku hadi siku.
Wema Sepetu katika pozi na washabiki wake mapema mchana huu.
Mastaa wetu wa filamu hapa nchini, wametokelezeaje sasaaa.
Kiongozi wa msafara wa tamasha la Serengeti Fiesta 2012,Mully B akiwa na mastaa wa filamu,Wema Sepetu na Aunt Ezekiel afu fulllll BBM kama kawa.
Millard Ayo akifanya mahojiano na Ray a.k.a Vincent Kigosi kuhusiana na ujio wao ndani ya  mji wa Moshi
Kutoka kushoto ni Mr Hatman,Steve Nyerere,Bonge pamoja na Millard Ayo katika shoo love ya pamoja.
Wakiwa katika mazungumzo yao ya hapa na pale.
Kila mmoja ana haki ya kupata habari na kuhabarishwa.
Pichani ni Gari aina ya Vits itakayotolewa jioni ya leo kwenye tamasha la Serengeti Fiesta 2012,kwa mshindi atakaejishindia kwenye droo itakayofanyika katika uwanja wa chuo cha ushirika,ambako tamasha hilo litarindima mpaka majogoo.
Jacob Steven a.k.a Steven akifafanua jambo mapema leo mtaa wa Malindi kuhusiana na suala zima la wasanii hao kulivamia jiji la Moshi

Thursday, August 23, 2012

Taharuki nchini Kenya baada ya mauaji


Baadhi ya watu wamelazimika kutafuta hifadhi sokoni kwa kuhofia usalama wao.
Tana River, Kenya
Tana River, Kenya
Mauaji hayo yalitokea wakati watu wenye silaha kutoka jamii ya Pokomo waliposhambulia kijiji kimoja katika eneo la Reketa huku wakiteketeza makaazi ya watu.
Mmoja wa wale walioathiriwa ameelezea BBC kwamba walishambuliwa usiku, ''hata tumekimbia kutoka kijiji chetu sasa. Walikuja kwa kijiji cha Riketa, watu walikuwa wanalala hata hawana habari wakavamia akina mama, watoto wote wamekufa hapa hapa.''
Alisema shambulizi hilo limewashangaza kwa sababu hata wakati mifugo wao wameingia kwenye mashamba, kuna njia ya kufidia, ''sisi kawaida yetu, hiyo mifugo inashikwa kisha unalipishwa. Sio kukatakata mifugo au kumaliza wachungaji.''
Naibu kamanda wa polisi mjini Mombasa, Joseph Kitur amesema uchunguzi wa awali umebainisha kuwa shambulio hilo lilifanywa na watu kutoka jamii ya Pokomo.
Jamii za Pokomo na Orma zimekuwa zikizozania malisho na maji tangu mwezi uliopita lakini shambulizi hili ndilo mbaya zaidi kutokea kati yao.
Mwaka wa 2001, karibu watu 130 walifariki wakati mzozo kati ya jamii hizo mbili ulipozuka.
Jamii ya Pokomo ni wakulima na huwa inategemea sana mto wa Tana kwa shughuli zao.
Jamii ya Orma ni wafugaji.
Mauaji hayo yameleta kumbukumbu za ghasia za baada ya uchaguzi za mwaka wa 2007, ambapo watu 1,200 walifariki katika mapigano.

Sunday, August 19, 2012

SALAMU ZA EID MUBARAK KUTOKA KWA MHE LOWASSA KWA WAISLAMU NA WATANZANIA WOTE

Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa.
LEO ni sikukuu ya Eid Elfitr, ambapo ndugu zetu Waislamu wameungana na Waislamu duniani kote kuishrehekea sikukuu hii tukufu iliyoanza baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Binafsi kwa niaba ya familia yangu na wananchi wote wa Jimbo la Monduli, Napenda kuchukua fursa hii kuwatakia Watanzania wote mkono wa Eid Elfitr.
Kwa wagonjwa na wenye shida mbalimbali nachukua pia fursa hii kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awape tahafifu ili kwa pamoja tusherehekee sikukuu hii tukufu kwa wenzetu Waislamu. 
Na pia Nawaombea mpate afuene ili kwa pamoja tuendelee na jukumu la pamoja la kuijenga nchi yetu pamoja na kumsaidia Mh Rais Jakaya Kikwete katika kuitekeleza vyema ilani ya Chama Chama Mapinduzi, ambayo inahimiza kuilinda amani ya nchi yetu kama tunu pekee tuliyorithi toka kwa waasisi wetu wa taifa Baba wa Taifa Mwalimu Julius K .Nyerere na Mzee wetu Sheikh Abeid Aman Karume. 
Ambapo leo hii dunia inajua na Tanzania inajua Amani tuliyonayo inatokana na misingi imara tuliyojengewa kama taifa na kufanikiwa kuheshimiana na kuvumiliana licha ya tofauti zetu za kikabila, kidini na kiimani, lakini wote tunaabudu bila kuvunja amani yetu na sheria za nchi.
Kwa pamoja naomba niwatakie siku njema na Asanteni sana Wanatanzia wenzangu

EID MUBARAK WOTE NAWAPENDA SANA...

Ajali ya ndege yamuuwa waziri Sudan

Wazir Ghazial Sadiq Abdelrahim aliuwawa ajalini
Waziri wa dini wa Sudan Ghazi al-Sadiq Abdel Rahim ni miongoni mwa watu 31 waliouwawa katika ajali ya ndege.
Shirika la habari la Sudan limesema kuwa mawaziri wengine wawili na pia viongozi wa chama kinachotawala cha Omar el-Bashir pia waliuwawa.
Ndege hiyo ya abiria ambayo pia ilikuwa imebeba wakuu kadhaa wa kijeshi ilianguka katika eneo la milima ya Nuba
Ndege hiyo ilikuwa ikielekea eneo la Kordofan ya Kusini kwa sherehe za Eid al-Fitr ili kuuaga mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Mbali na waziri huyo wa maswala ya kidini Ghazi al-Sadiq Abdel Rahim wengine waliofariki katika ajali hiyo ni mwenyekiti wa chama, Makki Ali Balayil, waziri wa vijana na michezo, na Issa Daifallah, waziri wa utalii na wanayma pori.
Ndege hiyo ilianguka katika eneo la Talodi huko Kordofan ya Kusini, ikiwa imetoka mji mkuu Khartoum
Mji huo wa Talodi, uko kilomita 50 kutoka mpaka wa Sudan Kusini.
Taarifa za runinga ya taifa zinasema kuwa hali mbaya ya anga iliizuia ndege hiyo kutua na ilipojaribu mara ya pili iligonga mlima.
Afisa mmoja wa shughuli za ndege alisema kuwa ndege hiyo ilikuwa ya aina ya Antonov.
Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ajali kadhaa mbaya za ndege.
Maafisa wa Sudan wamekuwa wakilalamika kuwa imekuwa vigumu wao kupata vipuri kwa sababu ya vikwazo vya Marekani.

Saturday, August 18, 2012

MWAKIFAMBA AWAPIGIA MAGOTI BONGO MOVIE

Simon Mwakifamba
Jacob Steven ‘JB’
Stori: Mwaandishi wetu
RAIS wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifamba, juzikati aliwapigia magoti wasanii wa Bongo Movie akijishusha na kuomba radhi kwa yote aliyokuwa akikwazana nao kabla ya kukaa chini na kuzungumza.
Tukio la kiongozi huyo kushusha goti chini kwa wasanii hao lilijiri Agosti 15, mwaka huu ndani ya Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar es Salaam, mara baada ya Mwakifamba kuanza kuhutubia kikao kilichokuwa na lengo la wasanii kuungana kupinga wizi wa kazi zao.
Mwakifamba alisema kuwa umefikia wakati wake wa kujishusha ili kuifanya tasnia hiyo kuwa kitu kimoja na waweze kutimiza malengo yao.
MSIKILIZE JAMAA ALIVYOSHUKA
“Ndugu zangu na wasanii wenzangu, leo ni siku ya pekee ambapo nafarijika kwa kukutana na umati wa wasanii wenzangu wa tasnia hii ya filamu, hivyo basi kufuatia mambo mengi yaliyokuwepo baina yetu,  leo napenda kuitambua rasmi Bongo Movie na kuomba radhi kwa yote mabaya niliyowahi kuyasema hapo nyuma.
“Baada ya kuomba radhi sasa nawaomba wasanii wote kuanzia leo hii tushikamane na tuweze kutokomeza wimbi la wizi wa kazi zetu,’ alisema Mwakifamba.
MWENYEKITI WA BONGO MOVIE ‘JB’ AMWONGELEA MWAKIFAMBA NJE YA JUKWAA
Akizungumzia kujirudi kwa Mwakifamba, Mwenyekiti wa Bongo Movie Club, Jacob Steven ‘JB’ alisema bosi mwenzake huyo amefanya jambo lenye heshima miongoni mwao na akasisitiza mshikamano baina yao kuanzia siku hiyo.
“Naweza kusema kuwa, Mwakifamba ameonesha jambo la heshima na kitendo chake cha kusema yaliyopita si ndwele tugange yajayo ni matokeo ya busara zake, tumempokea, tunaunga mkono mshikamano ili  wasanii tupige hatua, tunataka kupambana na wezi wa kazi zetu,” alisema JB.

NAPE AFUTURISHA WAJUMBE WA NYUMBA KUMI MOROGORO

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akikaribishwa na Kaimu Katibu wa CCM mkoa wa Morogoro Six Mapunda na Kada wa CCM na Hassan Bantu (kulia) alipowasili kwenye ukumbi wa shule ya sekondari ya Forest ambako aliandaa futari kwa ajili ya mabalozi wa nyumba kumi na baadhi ya viongozi wa CCM kutoka wilaya za mkoa wa Morogoro jioni hii ya jana Agosti 17, 2012.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akisalimiana kwa furaha na mkuu wa mkoa wa zamani wa Morogoro steven Mashishanga baada ya kuwasili kwenye futari hiyo iliyoandaliwa na Nape kwenye ukumbi wa Shule ya sekondari Forest mjini Morogoro.
Waalikwa wakisali kabla ya kufuturu futari hiyo iliyoandaliwa na Nape kwenye ukumbi wa Shule ya sekondari Forest mjini Morogoro.
Kina Baba wakifuturu futari hiyo iliyoandaliwa na Nape kwenye ukumbi wa Shule ya sekondari Forest mjini Morogoro.
Mashishanga, Fikiri juma wa mjini,Nape na wa mkoa petro kingu wakifuturu, futari iliyoandaliwa na Nape kwenye ukumbi wa Shule ya sekondari Forest mjini Morogoro.
Kaimu Katibu wa CCM mkoa wa Morogoro Sixtus Mapinda na Msaidizi wa  Katibu NEC, Itikadi na Uenezi, Taifa, Okctavian wakifuturu, futari hiyo iliyoandaliwa na Nape kwenye ukumbi wa Shule ya sekondari Forest mjini Morogoro.
Babu akijisevia futari, wakati wa futru hiyo iliyoandaliwa na Nape kwenye ukumbi wa Shule ya sekondari Forest mjini Morogoro.
Mkuu wa mkoa Moro Joel Bendera akifuturu,futari hiyo iliyoandaliwa na Nape kwenye ukumbi wa Shule ya sekondari Forest mjini Morogoro.
Kina mama wakifuturu, futari hiyo iliyoandaliwa na Nape kwenye ukumbi wa Shule ya sekondari Forest mjini Morogoro.
Six akimkaribisha Nape jukwaani baada ya kufuturu, futari hiyo iliyoandaliwa na Nape kwenye ukumbi wa Shule ya sekondari Forest mjini Morogoro.
Nape akizungumza jukwaani, baada ya futari hiyo aliyoandaa kwenye ukumbi wa Shule ya sekondari Forest mjini Morogoro.
Nape akizungumza jukwaani baada ya futari hiyo.
Sheik  Khamis Ali Mbilikila akisoma dua baada ya futari hiyo iliyoandaliwa na Nape kwenye ukumbi wa Shule ya sekondari Forest mjini Morogoro.
Nape akishiriki kuomba dua baada ya futari. Kulia ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Morogoro
Kina mama wakiomba dua
Kinababa wakiomba dua
Nape, Bendera na Kingu wakiwa wamesimama baada ya futari hiyo.
Nape akiwaaga waalikwa
Nape na mbunge wa zamani Simeindu Pawa wakisalimiana baada ya futari hiyo
Nape akiagana na mjumbe wa nyumba kumi  Zuberi Fikirini baada ya futari. Mjumbe huyo ni mlemavu wa miguu

--

Tuesday, August 14, 2012

MASTAA WADAIWA KUJIUZA BBM

Hamida Hassan na Gladness Mallya
BAADHI ya mastaa Bongo wanadaiwa kuwa na tabia ya kutumia mtandao wa simu wa BlackBerry Messenger ‘BBM’ vibaya ikiwa ni pamoja na kujiuza kwa wanaume, Ijumaa limebaini.
Utafiti uliofanywa na mapaparazi wetu umeonesha kuwa, wapo ambao wawapo vyumbani kwao hujipiga picha za utupu na kuzitupia kwenye mtandao huo kisha baada ya muda huzitoa.
Wakizungumzia tabia hiyo, baadhi ya wanaume wanaotumia BBM walikiri kukumbana na picha hizo za ajabu za mastaa huku zikiambatana na maneno ya kujitongozesha kwao.
“Huyu …(anataja jina la staa maarufu Bongo), juzi usiku mishale ya saa nane alianza kunitumia ‘sms’ kuniuliza kama niko macho. Nilipomjibu akaniambia kuna zawadi anataka kunipa, nilivyomkubalia akatupia picha yake akiwa kitandani mtupu.
“Hazikupita hata sekunde nyingi, kabla ‘sijai-download’ akaitoa kisha akaniuliza nimejisikiaje kumuona alivyo. Nilishangaa lakini nikamjibu kwa kifupi kuwa ana mvuto, basi kuanzia siku hiyo akawa ameniganda,” anasema kijana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Sule ambaye ni mfanyabiashara jijini Dar.
 Msanii mwingine wa kiume aliyeomba hifadhi ya jina lake alisema:
“Mbona huo ndiyo mchezo wao, yaani ukishamkubalia kuwa rafiki yao basi subiri vituko, kwa kifupi sasa hivi wengi wanajiuza kupitia BBM.”
Katika kupata ukweli juu ya habari hiyo, waandishi wetu walizungumza na baadhi ya mastaa wa Kibongo wanaotumia mtandao huo ambapo walikuwa na haya ya kusema:

JACQUELINE PATRICK
Modo huyo mwenye jina kubwa Bongo alifunguka: “Kwa upande wangu siwezi kukataa kuwa sijawahi kuweka picha kama hizo, mimi ni mpenzi sana wa picha na ninaupenda sana mwili wangu hivyo nikipiga picha ya aina yoyote  lazima niitupie kwani ‘fansi’ wangu ndiyo wanaoweza kuniambia kama nimenenepa au nimekonda au kunisifia.
“Suala la kutongoza wanaume naweza nikasema kuwa mimi siweki kwa sababu hiyo kwani marafiki zangu wote kwenye BBM wana wapenzi wao.”

ZUWENA MOHAMED ‘SHILOLE’
Mwigizaji huyo ambaye pia ni mwanamuziki alisema: “Mimi sijawahi kumtongoza mwanaume na siwezi kwa sababu mila za kwetu zinasema mwanaume ndiye anatakiwa kumtongoza mwanamke hivyo mwanamke anayemtongoza mwanaume anakosea kwani ataonekana wa bei rahisi sana.
Labda wenzangu wanaweza kufanya hivyo kupitia njia hiyo.”

MIRIAM JOLWA ‘JINI KABULA’
Mwigizaji huyo alifunguka: “Mimi nina mume wangu, nampenda sana na mara nyingi siingii BBM ila ninauzisha tu picha zangu kule lakini kuchati na watu siyo kivile na siwezi kumtongoza mwanaume kwa sababu wanaume wanaopatikana kwa njia hiyo siyo kabisa labda mastaa wenzangu, lakini mimi sijawahi kumtongoza mwanaume.”

RACHEL HAULE ‘RECHO’
Staa huyo wa filamu alisema: “Sijawahi kumtongoza mwanaume ila suala la kutongozwa na wanaume kwenye BBM ni la kawaida, inategemea na msimamo wa mtu. Najua BBM tumejiunga kwa ajili ya kujua matukio yanayotokea kwa haraka zaidi na siyo kwa ajili ya kujiuza.”

ISABELA MPANDA
Mwigizaji huyo alitiririka: “Katika orodha ya hao wanaojiuza kupitia mtandano huo, mimi simo. Nipo BBM ila sijawahi kumtongoza mtu wala kutupia za utupu.”

RUTH SUKA ‘MAINDA’
Mwigizaji huyo mkongwe alisema: “Ni kweli nimejiunga BBM lakini kwa sasa nipo ‘shouting’ nicheki baadaye.
Mastaa wengine waliotajwa kuwepo BBM nja na waigizaji Aunt Ezekiel, Irene Uwoya, Agnes Gerard ‘Masogange’ na wengineo.

Monday, August 13, 2012

Tanzania itafuta sajili ya meli za Iran


Serikali ya Tanzania inasema meli za mafuta 36 za Iran zimesajiliwa tena nchini Tanzania, ili kujaribu kuhepa vikwazo dhidi ya Iran vilivowekwa na Marekani na Umoja wa Ulaya.
Meli ya mafuta ya Iran
Uchunguzi uliofaywa na serikali ya Tanzania, ambao ulionekana na shirika la habari la Reuters, unaonesha kuwa serikali haikujua lolote kuhusu shughuli hizo za kuzipatia meli za mafuta za Iran bendera ya Tanzania - shughuli iliyokuwa ikifanywa na wakala alioko Dubai.
Mafuta ya Iran yamewekewa vikwazo, ili kuishawishi Iran iache mradi wake wa nuklia.
Tanzania imeacha kuagiza mafuta kutoka Iran.
Uchunguzi ulifanywa na serikali ya Tanzania, baada ya mbunge mmoja wa Marekani, Howard Berman, mwenyekiti wa kamati ya Congress ya maswala ya nchi za nje, kueleza wasiwasi wake juu ya meli hizo za Iran kupatiwa bendera ya Tanzania.
Tanzania sasa inasema itafuta usajili wa meli hizo.

Helikopta za kivita za Uganda zapatikana

 
Msemaji wa Jeshi Uganda ,Kanali Felix Kulaigye
Jeshi la Uganda limesema kuwa helikopta zake nne zilizokuwa zime ripotiwa kutoweka zikiwa njiani kuelekea nchini Somalia sasa zimepatikana na marubani wake wote wako salama.
Akizungumza na BBC msemaji wa jeshi hilo Kanali Felix Kulaigye hakuweza kusema ndege hizo ziko wapi kwa sasa.
Naye msemaji wa jeshi la Kenya, Bogita Ongeri ameiambia BBC kwamba operesheni ya kutafuta ndege hizo ilikuwa imevurugwa na hali mbaya ya hewa na kuongeza kuwa helikopta hizo nne zilikuwa kwenye safari hiyo kutoka nchini Uganda.
Moja ya helikopta hizo ilitua katika mji wa Garissa.
Rubani aliyekuwa kwenye helikopta ya pili alizungumza na mamlaka za kenya akisema yuko katika eneo la mlima kenya lakini hakukukuwa na mawasiliano na helikopta nyingine mbili.
Helikopta hizo za Uganda hutumiwa kusindikiza misafara kutoka angani, katika opereresheni za utafutaji na uokoaji pamoja na kushambulia wanamgambo wa kiislamu wa Al Shabaab nchini Somalia.
Helikpta hizo ni miongoni mwa ndege ambazo zilikuwa zikielekea Somalia kukipa nguvu kikosi cha Umoja wa Afrika .
Awali msemaji wa jeshi la Uganda Kanali Felix Kulayigye alikuwa amesema kuwa walikuwa wakizitafuta ndege zao mbili aina ya Mi-24 . Alisema ndege hizo ni zile za kufanya mashambulizi.

Wednesday, August 1, 2012

MAELEZO BINAFSI YA MHE. ZITTO ZUBERI KABWE DHIDI YA TUHUMA ZA RUSHWA HUSUSAN KUELEKEA KATIKA KUPITISHA BAJETI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI

MAELEZO BINAFSI YA MHE. ZITTO ZUBERI KABWE DHIDI YA TUHUMA ZA RUSHWA HUSUSAN KUELEKEA KATIKA KUPITISHA BAJETI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI
Ndugu Waandishi,
Nalazimika kukutana nanyi kutoa maelezo juu ya tuhuma zenye shinikizo la kisiasa zinazoelekezwa kwangu binafsi kwamba hata mimi nimeshiriki katika vitendo vya rushwa, kwa nafasi yangu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma. Taarifa hizo, kama kawaida ya uzushi mwingine wowote  zimesambazwa kimkakati na kwa kasi kubwa kiasi cha kuukanganya umma.
Nafahamu nabeba dhamana kubwa ya uongozi, taswira yangu ya uongozi daima imeakisi njozi na matumaini ya wananchi wa Kigoma Kaskazini, wananchi wanyonge na vijana kote nchini bila kujali itikadi zao za kisiasa, jinsia zao, makabila yao na rika zao. Hivyo, nawajibika kupitia kwenu kuwatoa hofu juu ya hisia potofu zinazopandikizwa kwao na wale wasiopenda kuona baadhi yetu tukiwaunganisha na kuwasemea watanzania wasio na sauti, dhidi ya vitendo vya hujuma na vyenye dhamira ovu kwa taifa.
Mkakati huo wa kuniunganisha na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanaotuhumiwa kwa kupokea Rushwa unatekelezwa kwa njia zifuatazo:
  1.   Kumekuwa na kauli za watendaji wa serikali ambao wamekuwa wakizieneza na hususan kutoa taswira kwamba baadhi ya kauli zangu zinatokana na ushawishi wa rushwa;
  2.   Kuna taarifa ambazo zimeandikwa tena katika kurasa za mbele za baadhi ya vyombo vya habari  zikidai ’’Zitto kitanzini’’ ama ’’Zitto sawa na popo nundu’’  zikiashiria kwamba na mimi ni mla rushwa; na
  3.   Waandishi wa habari na jamii kwa ujumla wamefikia kuaminishwa habari hizi kiasi cha wengine kuuliza kwa nini Mhe. Zitto Kabwe hakutajwa katika orodha iliyotolewa na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani.
Ndugu Waandishi,
Naomba kutoa ufafanuzi wa hicho kinachoelezwa kwamba nina ushiriki katika masuala ya rushwa hususan kwenye masuala yanayohusu sekta ya Nishati na Madini:-
  1. Mara baada ya bodi ya Wakurugenzi ya  Shirika la Usambazaji wa Umeme Tanzania (TANESCO) chini ya Uenyekiti wake Meja Jenerali Mstaafu Robert Mboma kutangaza kwamba imemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Nd. William Mhando ili kupisha uchunguzi wa baadhi ya vitendo/mwenendo wake, Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ambayo mimi ni Mwenyekiti wake ilimuandikia Mhe. Spika kumuomba aridhie ili Kamati iweze kuwaita Bodi ya TANESCO, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali  (CAG) na pia Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kujiridhisha na tuhuma zote zinazotajwa zinafanyiwa uchunguzi wa kina na hatua kuchukuliwa;
  2. Kamati ya POAC ninayoiongoza ilimuomba Mhe. Spika kuwaita wahusika tajwa kwa kuwa zilikuwapo tetesi kuwa kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi huyo siku chache kabla ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kulikuwa na lengo la kufunika ’madudu’ makubwa zaidi kwa kulichagiza Bunge na tukio hilo dogo, mkakati ambao naona umefanikiwa sana. Isitoshe, Kamati kutaka kujiridhisha na hatua za Bodi ni sehemu ya msingi ya utekelezaji wa majukumu ya Kamati yaliyowekwa kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge na pia Shirika la TANESCO ni moja kati ya mashirika ambayo yanawajibika kwetu kwa hesabu zake na pia ufanisi wake kwa ujumla. Tumefanya hivyo pia katika mashirika mengine, hili la TANESCO sio tukio la kipekee;
  3. Kitendo hiki cha halali na kwa mujibu wa Kanuni kilichofanywa na Kamati yangu  kimetafsiriwa kwa makusudi na baadhi ya watu kwamba ni ishara ya kuwa sisi au zaidi kwamba mimi nina maslahi binafsi na TANESCO na hususan Mkurugenzi wake Injinia Mhando, ndio maana tumetaka maelezo ya Bodi. Ukweli kwamba Kamati ya POAC tumewaita pia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu (CAG) na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kwa jambo hilo hilo umefichwa kwa makusudi!
  4. Baada ya  tukio hilo, nikiwa hapa Dodoma, mwandishi wa habari wa gazeti moja alinifuata akiniambia kuwa wamekutana na Mhe. Waziri Mhongo na Katibu Mkuu wake, Nd. Eliachim Maswi hapa hapa Bungeni na wamewaambia kuwa mimi nimepewa rushwa. Hakutaja nimepewa rushwa na nani, kiasi gani na wala kwa lengo gani!
  5. Nimejaribu kumtafuta kwa simu Mhe. Waziri Mhongo na Katibu Mkuu wake ili wanipe ufafanuzi juu ya mimi na Kamati ya POAC kuhusishwa na tuhuma hizi bila mafanikio, hali ambayo inaniondolea mashaka juu ya ushiriki wao katika kueneza au kuthibitisha uvumi huo. Najaribu sana kujizuia kutokuwa na mashaka na ushiriki wao huo ikizingatiwa uzito na taswira ya nafasi zao katika jamii, lakini wameshindwa kunidhihirishia tofauti.
Sasa naomba kutoa ufafanuzi rasmi kuhusu mlolongo wa matukio hayo tajwa ambayo yanatumiwa na baadhi ya wanasiasa kuonesha kwamba eti nimehusika na vitendo vya rushwa.
  1. Binafsi sijawahi kuwa na mawasiliano ya aina yeyote na uongozi wa TANESCO kushawishiwa juu ya hatua ambazo POAC ndio imezichukua za kutaka kujiridhisha juu ya utaratibu uliotumika. Ieleweke wazi kabisa kuwa, hakuna wakati wowote, popote ambapo mimi binafsi au Kamati yetu imekataa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO kuchunguzwa kwa tuhuma zozote. Ambacho tumesisitiza wakati wote ni ufuatwaji wa taratibu, kanuni na sheria, hili nitalisimamia iwe masika au kiangazi;
  1. Ni kwa sababu hiyo, na kwa kujiamini kabisa nimeunga mkono suala la tuhuma za rushwa zinazotajwa zichunguzwe na Kamati ya Haki, Maadili na  Madaraka  ya  Bunge kwa kina;
  1. Nimekwenda mbali zaidi kukiomba chama changu CHADEMA kifanye pia uchunguzi na tathmini yake kwa kina kujiridhisha na tuhuma hizo;
  1. Natumia fursa hii pia kuomba vyombo vya Dola vichunguze tuhuma hizo kwa nafasi yake ili kuweza kupata ukweli;
  1. Ninaahidi kushiriki kikamilifu iwapo nitatakiwa katika uchunguzi wowote utakaofanywa na niko tayari kuwajibika iwapo nitakutwa na hatia yeyote.
Napenda niwatoe hofu wananchi wa jimbo la Kigoma Kaskazini walionituma kuja kuwawakilisha hapa Bungeni na Watanzania wote kwa ujumla kwamba:-
  1. Mimi Zitto Zuberi Kabwe sina bei, sijawahi kuwa nayo na sitarajii kuwa nayo huko mbeleni. Daima nimesimamia kidete maadili ya uongozi bora katika maisha yangu yote ya siasa, na nawaahidi sitarudi nyuma katika mapambano dhidi ya rushwa katika nchi hii pamoja na mikakati ya aina hii ya kunidhoofisha na kunivunja moyo;
  1. Nafarijika na salam mbali mbali zinazotolewa kunifariji na kusisitiza kuwa nisilegeze kamba katika mapambano haya, nimepokea ujumbe mwingi kwa simu, sms, tweeter na hata facebook na niko pamoja nanyi Watanzania wenzangu kamwe sitarudi nyuma hadi kieleweke. Naamini katika nchi yetu tunazo rasilimali za kutosha mahitaji/haja ya kila mmoja wetu lakini si ‘tamaa/ulafi’ wa baadhi ya watanzania wenzetu;
  1. Napenda kuweka rekodi sawa kwa Watanzania kwamba nimekuwa Mbunge hiki ni kipindi cha pili, Mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) huu ni takriban mwaka wa saba sasa, Kamati yangu inasimamia mashirika 259 ya Umma na si TANESCO peke yake. Mchango wa Kamati hii katika Bunge na kwa ustawi wa Mashirika ya Umma ni bayana na haujawahi kutiliwa shaka. Kamati yetu imeokoa upotevu mkubwa wa mali za umma na kuokoa fedha za umma kutokana na umakini wake. Tumefanya hivyo CHC hivi karibuni, Kiwira na kwenye mashirika mengine mengi. Kote huko uadilifu na uzalendo wa Kamati hii haujawahi kuhojiwa. Inatuwia vigumu kuona kuwa tunahojiwa katika suala hili la TANESCO. Hapa pana kitendawili.
  1. Zipo hoja pandikizi za kutaka Kamati ya POAC ivunjwe na haswa zikinilenga mimi binafsi. Nafahamu kiu ya wasioitakia mema nchi yetu kuiona POAC ikivunjwa au sura zikibadilishwa kwa kuwa Kamati hii imekuwa mwiba kwa mikakati yao ya kifisadi. Kwa maoni yangu, Kamati ya POAC isihusishwe na tuhuma hizi kwa vyovyote vile. Niko tayari nihukumiwe mimi kama mimi na sio kuhusisha wajumbe wengine ambao hawatajwi mahala popote katika tuhuma hizi mbaya sana katika historia ya Bunge letu. Nitakuwa tayari kunusuru Kamati ya POAC na maslahi ya taifa letu kwa kujiuzulu Uenyekiti iwapo itathibitika pasipo shaka kuwa nimehongwa. Kamati ya POAC ni muhimu zaidi kuliko mimi.
  1. Nafahamu pia kuwa kuna wanasiasa hasa wa Upinzani ambao wanautaka sana Uenyekiti wa POAC na wanafanya kila njia kutaka kuidhoofisha. Lakini hawajui kuwa anaepanga wajumbe wa Kamati ni Spika wa Bunge.
  1. Msishangae pia kuja baadae kubaini kwamba baadhi ya wanasiasa wenye midomo mikubwa ya kutuhumu wenzao wao ndio vinara wa kupokea rushwa.
  1. Ni lazima tufike mahali kama viongozi kwamba utaratibu unapokiukwa na yeyote yule, au uongo unapotolewa hadharani tuseme bila kuogopa. Hili ndio jukumu letu kama wabunge na viongozi. Kusimamia ufuatiliaji wa utaratibu ni jukumu letu kama Kamati ya POAC na ndio sababu ya msingi ya kuanzishwa kwa mamlaka kama CAG na PPRA. Haiwezekani, tuwe na set ya kanuni kwa kundi fulani na nyingine kwa makundi mengine, au kuhukumu ufuataji wa taratibu kwa kuangalia sura ya mtu usoni
Mwisho
Kumejengeka tabia hivi sasa ya kuwamaliza wanasiasa wenye kudai uwajibikaji na uzalendo. Kumeanzishwa kiwanda kwenye medani ya siasa cha kuzalisha majungu na fitna zenye lengo la kuwachonganisha wanasiasa wa aina hiyo na wananchi kwa kutumia vyombo vya habari na nguvu ya fedha. Naamini mbinu hizi chafu, kama nyingine nyingi zilizojaribiwa kwangu huko nyuma nazo zitashindwa.
Naamini katika kweli na kweli daima huniweka huru. Naamini kuwa mwale mdogo wa mwanga wa mshumaa hufukuza kiza. Kwa imani hiyo, sitasalimu amri mbele ya dhamira zao ovu hata nitakapobaki peke yangu katika mapambano hayo ya kulinda na kutetea rasilimali za taifa zinufaishe watanzania wote.
Daima nitaongozwa na busara ya Hayati Shabaan Robert isemayo, ‘Msema kweli huchukiwa na marafiki zake, nitakapofikwa na ajali hiyo, sitaona wivu juu ya wale wawezao kudumu na marafiki zao siku zote, siwezi kuikana kweli kwa kuchelea upweke wa kitambo, nikajitenga na furaha ya kweli itakayotokea pale uwongo utakapojitenga”.
Ahsanteni sana.

Zitto Zuberi Kabwe