Dwain Chambers sasa anaweza kushiriki katika mashindano ya
London 2012, kufuatia uamuzi wa mahakama ya kimataifa ya rufaa inayohusika na
michezo duniani, Court of Arbitration for Sport (Cas).
Chama cha Olimpiki cha Uingereza, BOA, kimekuwa na sera ya kuwazuia maisha
wanariadha wanaoadhibiwa kwa kutumia dawa za kuongezea nguvu michezoni
kutoshiriki katika mashindano.Chama hicho cha Olimpiki kimeshindwa kuitetea sera hiyo iliyopingwa na chama cha dunia cha kupambana na dawa za kuongezea nguvu michezoni (World Anti-Doping Agnecy), kwa kifupi Wada, mzozo ambao ulifikishwa mbele ya mahakama ya kimataifa inayohusika na michezo,
Uamuzi wa mahakama hiyo unamaanisha kwamba Dwain Chambers, mwenye umri wa miaka 34, na mweneshaji baiskeli David Millar, mwenye umri wa miaka 35, wote kama Waingereza, wanaweza kufuzu kujiunga na timu ya taifa, maarufu kwa jina Team GB.
Mahakama ya kimataifa ya kesi za michezo inatazamiwa rasmi kutangaza uamuzi wake Jumatatu, saa kumi na moja alasiri.
Hata hivyo wanariadha watawajibika kufuzu katika mashindano ili kufikiriwa kama itawezekana kujiunga na timu ya taifa.
Wanamichezo wa Uingereza ambao daima dawama wamekatazwa na chama cha Olimpiki cha Uingereza kushiriki katika mashindano ya Olimpiki katika maisha yao yote ni Dwain Chambers, David Millar, Carl Myerscough, Peter Meakin, Jade Mellor, Callum Priestley, Dan Staite na Jamie Stevenson.
Chambers aligunduliwa kutumia dawa aina ya THG mwaka 2003, na aliadhibiwa asishiriki katika mashindano ya riadha kwa miaka 2, na mwaka mmoja baadaye, Miller naye alipewa adhabu hiyohiyo, baada ya kukiri kutumia dawa ya kuongezea damu nguvu ya EPO.
Wanariadha wote wawili tangu wakati huo wameshirikiana na maafisa mbalimbali wa kupambana na kuzuia utumizi wa dawa za kuongezea nguvu michezoni.
Chama cha Olimpiki cha Uingereza kimekuwa kikijitetea kwamba kina haki ya kuamua kuwazuia maisha Waingereza wanaogunduliwa kutumia dawa za kuongezea nguvu, hata baada ya wanamichezo hao kukamilisha adhabu waliopewa, jambo ambalo limekuwa likipingwa na Wada.
Wakuu wa chama cha Olimpiki cha Uingereza waliifikisha kesi hiyo mahakamani kupinga msimamo wa Wada.
Wada ilikuwa imesema sera ya chama cha Olimpiki cha Uingereza haiambatani na kanuni za Wada.
Sheria hiyo ya chama cha Olimpiki cha Uingereza, ambayo imekuwepo kwa zaidi ya miaka 20, imewazuia wanamichezo wengi kushiriki katika mashindano ya Olimpiki yaliyopita.
No comments:
Post a Comment