Fernando Torres amepachika mabao matatu murua na kuweka hai
matumaini ya Chelsea kumaliza katika nafasi nne za juu za msimamo wa Ligi Kuu ya
Kandanda ya England, walipoilaza QPR mabao 6-1 ambao wapo hatarini kushuka
daraja.
Torres alikamilisha mabao yake matatu baada ya mapumziko na Florent Malouda akafunga kitabu kwa kuandika bao la sita kabla ya Djibril Cisse kuipatia QPR bao moja la kufutia machozi.
Matokeo hayo yameibakisha Chelsea katika nafasi ya sita huku QPR ikiwa juu ya mstari wa kuteremka daraja kwa tofauti ya mabao na Bolton.
Katika mchezo mwengine Tottenham imefanikiwa kujiinua hadi nafasi ya nne ya msimamo wa Ligi Kuu ya Kandanda ya England baada ya kuilaza Blackburn mabao 2-0. Blackburn wana wasiwasi mkubwa wa kuteremka daraja msimu huu na kufungwa kwao kumewazidishia hofu hiyo.
Rafael van der Vaart alitangulia kuipatia Spurs bao la kwanza kwa kwaju wa karibu baada ya mpira wa kichwa uliopigwa na Gareth Bale kugonga mwamba wa lango la Blackburn.
Kyle Walker akiwa umbali wa yadi 25 aliachia mkwaju wa adhabu ya moja kwa moja na mpira ukaenda moja kwa moja wavuni na kuipatia Spurs bao la pili dhidi ya Rovers ambao wapo nafasi ya pili kutoka mkiani na hawakuonesha mchezo wowote wenye nia ya ushindi.
No comments:
Post a Comment