Monday, May 7, 2012

Manchester City yajiwekea mazingira safi...soma zaidi

Manchester City imesogea karibu kabisa ya mfundo wa kumalizia Ligi Kuu ya Engald na kutangazwa mabingwa kwa mara ya kwanza baada ya miaka 44, baada ya Yaya Toure kufunga mabao mawili na kuipatia ushindi wa mabao 2-0 timu yake dhidi ya Newcastle United.
Yaya Toure akishangilia moja ya mabao yake
Yaya Toure akishangilia moja ya mabao yake
Kiungo huyo anayechezea pia timu ya taifa ya The Ivory Coast alifanikiwa kumfunga mlinda mlango Tim Krull kwa mkwaju maridadi wa kimo cha beberu zikiwa zimesalia dakika 20 kabla mpira kumalizika.
Baadae kidogo Yaya Toure akaongeza bao la pili kwa mkwaju wa karibu huku muda nao ukiwa umewatupa mkono Newcastle.
Manchester City sasa wanafahamu fika iwapo watafanikiwa kupata ushindi dhidi ya QPR katika mechi ya kumalizia msimu, basi watatangazwa moja kwa moja mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya kandanda ya England.
Ulikuwa ni mchezo murua hasa kwa Manchester City wakiongozwa na nahodha wao Vincent Kompany safu ya ulinzi, huku David Silva akitawala eneo la kiungo na umaliziaji uliofana wa Toure akishirikiana na kikosi kizima wakihakikisha hawafanyi makosa kulikosa kombe msimu huu.
Ulikuwa uwanja huo huo wa Newcastle tarehe 11 mwezi wa Mei mwaka 1968 ambapo Manchester City walinyakua ubingwa wa ligi kwa mara ya mwisho. Takriban miaka 44 baadae inaonekana historia ipo njiani kujirudia huku klabu hiyo ikisogea mbele ya Manchester United ambao waliokuwa wanaongoza ligi hiyo kwa muda mrefu.
Clint Dempsey akiwa amefunga bao lake la 23 msimu huu aliisaidia timu yake ya Fulham kupata ushindi murua wa mabao 2-1 dhidi ya Sunderland.
Dempsey alipachika bao kwa mkwaju wa free-kick umbali wa yadi 25 na kuwa bao la pili lililoipatia ushindi Fulaham na kuipaisha hadi nafasi ya nane ya msimamo wa Ligi.
Djibril Cisse akiingia mchezaji wa akiba aliiongezea uhai dakika za mwisho timu yake ya Queens Park Rangers iepuka panga la kushushwa daraja baada ya hatimaye kufanikiwa kuwalaza Stoke bao 1-0 walioonyesha ubishi katika uwanja wa Loftus Road.
Cisse akiwa amesahauliwa na walinzi wa Stoke alipokea pasi ya Anton Ferdinand akiwa karibu na lango na akaweka mpira kimiani na kuwasukuma Bolton chini yao na wao kujikwamua eneo la kushuka daraja.
Thomas Sorensen mlinda mlango wa Stoke awali aliwanyima nafasi za kufunga Taarabt na Cisse.
Lakini hali ingekuwa tofauti kama Cameron Jerome wa Stoke angefanikiwa kupachika bao baada ya mkwaju wake kupiga nyavu ndogo dakika za mapema.
Tottenham nao wamepoteza nafasi ya kujisogeza hadi nafasi ya tatu wakati Aston Villa walipofanikiwa kupunguza hofu yao ya kushuka daraja kwa timu hizo kugawana pointi moja baada ya kufungana bao 1-1.
Ciaran Clark alikuwa wa kwanza kuipatia Villa bao kwa mkwaju alioufyatua kutoka yadi 25 uliomgonga mlinzi William Gallas na kujaa wavuni.
Gareth Bale alinyimwa nafasi ya kupachika bao na mlinda mlango wa Villa Shay Given aliyekuwa macho langoni lakini mlinzi wa Spurs Danny Rose baadae alitolewa nje kwa kadi nyekundu kwa rafu mbaya dhidi ya Alan Hutton.
Hata hivyo baadae Richard Dunne alimchezea rafu Sandro ndani ya sanduku la hatari na Emmanuel Adebayor akasawazisha kwa mkwaju wa penalti na hali iliyowabakisha nafasi ya nne nyuma ya Arsenal kwa pointi moja tu.
Wolves nao walifanikiwa kufuta rekodi ya kufungwa mechi ya 10 mfululizo nyumbani kwao baada ya kulazimisha sare ya kutofungana dhidi ya Everton.
Everton walifanikiwa kumiliki mpira muda mrefu wa kipindi cha kwanza huku Nikica Jelavic akipachika bao ambalo mwamuzi alilikataa kutokana na mshambuliaji huyo kuwa ameotea na pia Steven Pienaar naye alikosa nafasi nyingi za kufunga.
Wolves walijirekebisha kipindi cha pili lakini Everton bado waliendelea kuwa hatari langoni mwao huku Jelavic akipoteza nafasi nzuri ya kufunga.
Hata hivyo Wolves ambao wameshateremka daraja walifanikiwa angalao kupata pointi moja ya kwanza kwenye uwanja wao tangu tarehe 4 mwezi wa Desemba.
James Morrison akiingizwa kipindi cha pili alifanikiwa kuisawazishia West Brom ambao tayari walikuwa wameshafungwa mabao 2-1 na Bolton waliokuwa wakihaha kujinasua eneo la kushushwa daraja.
Martin Petrov alikuwa wa kwanza kuipatia bao Bolton kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 24 kufuatia rafu iliyochezwa na Keith Andrews.
Bolton waliongoza kwa mabao 2-0 baada ya Billy Jones wa West Brom kujifunga mwenyewe, lakini baadae Chris Brunt na Morrison wakafanikiwa kusawazisha mabao yote.

No comments:

Post a Comment