Msanii ambaye hajawahi kukaukiwa na matukio yenye kufaa kutengeneza
vichwa vya habari katika vyombo vya habari nchini, Wema Abraham Sepetu,
kwa mara nyingine ametawala vyombo vya habari baada ya tukio lake la
usiku wa jana la kuvishwa pete ya uchumba na msanii wa bendi ya Machozi,
anayekwenda kwa jina la Mwinyi.
Tukio hilo ambalo limevuta hisia za wapenzi wa masuala ya udaku na
burudani nchini, lilijiri katika ukumbi wa Maisha Club, jijini dar es
salaam, usiku wa kuamkia leo, ambapo lilishuhudiwa na mashabiki lukuki
wa bendi ya Machozi waliokuwa wamejazana hapo kwa ajili ya burudani ya
muziki uliokuwa ukiporomoshwa na bendi hiyo.
Hata hivyo, tofauti na ambavyo imechukuliwa na watu wengi kuwa Wema
amepata mchumba mpya na ndio alikuwa akimvisha rasmi pete ya uchumba,
ukweli ambao umewekwa wazi ni kuwa, mwanadada huyo alihusika katika
tukio hilo kama sehemu ya maandalizi ya filamu yake mpya itakayokwenda
kwa jina la Super Star.
Movie hiyo inatarajiwa kuelezea maisha halisi ya msanii huyo ambaye
pia aliwika katika medani za ulimbwende, na Mwinyi atashiriki katika
filamu hiyo akiigiza nafasi ya mwanamuziki Diamond, ambaye alikuwa
mpenzi wa Wema na ambaye alimvisha pete ya uchumba lakini wakamwagana
baadae kutokana na mikasa baina yao kuzidi kushamiri.
Kibwagizo: Hata hivyo, Wema anajulikana kuwa hajatulia, unadhani
itashangaza kesho kusikia kuwa tukio hilo mbali ya kuwa sehemu ya
filamu, lilikuwa pia tukio rasmi la kuwaunganisha wawili hao?