Tuesday, May 22, 2012

TUNATOA POLE KWA WADAU WOTE KUFATIA KIFO DOKTA VEDASTO KYARUZI ALIYEBUNI JINA LA TANZANIA NA ALIWAHI KUWA RAIS WA TAA. MIAKA YA 50.

 Mdau Erick akimlisha keki  dokta Kyaruzi wakati wa uhai wake.

MAKALA   YA MDAU UPENDO ERICK BAADA YA KIPO CHA DOKTA KYARUZI
Si watanzania wengi sana wa kizazi cha miongo baada ya Uhuru wanaomfahamu au wamesikia habari za Dokta Vedasto Mzungu Kyaruzi, Mtanzania Mzalendo na Mwanamapinduzi, Msomi wa awali wa kiwango cha Udaktari wa Binadamu ndani ya Tanganyika. Nafasi ya wengi kumjua Dokta Kyaruzi imepotea kutokana na kuwa na Taifa lisilo na misingi mizuri ya kutambua michango na kuona ufahari juu ya uzalendo wa  watu wake.

Ninamshukuru Mungu kwa kunipa nafasi ya kuwa karibu na Dokta Kyaruzi. Amekuwa rafiki na mlezi wangu; akiningoza vema jinsi ya kukua kitaaluma, kuishi na watu, makundi na jamii mbalimbali. Nakumbuka wakati wa hafla ya kunipongeza kwa kuhitimu Shahada ya Kwanza, Dokta aliniusia kwa msisitizo kwamba; Waafrika wengi wanadhani kuhitimu masomo ndo mwisho wa elimu katika fani husika. Kwake kuhitimu kulimaanisha mwanzo mpya wa kusoma fani kiundani zaidi, kujisajiri katika Journals, Periodicals, na Newsletters ili kuhakikisha anakwenda sambamba na kukua kwa maarifa katika tasnia yake. Ndipo alipopata kunijulisha maana ya neno “Practitioner” linalowekwa mbele ya vyeo vya Madaktari, Wahasibu, Wanasheria na fani zingine huko kwenye nchi zilizoendelea.

Pia, daima Daktari hakuacha kuniusia juu ya siasa na nafasi ilipotokea alinikutanisha na wanasiasa wakongwe mmoja wapo akiwa ni marehemu Abdulnoor Suleiman. Siku zote aliniambia na kunikanya kuwa, kama nia ya mtu kujiunga na siasa ni kujilimbikizia mali basi mtu huyo amekosea njia maishani.  Katika ushiriki wake kwenye siasa, alithamini sana haki iliyompa mtu uhuru maishani kuliko mali ambayo ingemkosesha amani na heshima kwenye jamii. Mara kwa mara alisema; mtu akigonga mlango wa nyumba yake usiku wa manane atajua ama ni jirani kapata shida au kuna mtu anataka maelezo kapotea njia. Hawezi kuogopa kama wanasiasa wa siku hizi walafi ambao likiwatokea haraka uhisi “mambo yameharibika”. Mbele ya nyumba yake mara nyingi alijipumzisha Mbeba-Mkaa, Mlevi aitwaye Rostamali. Dokta alipenda kumtumia Rostamali kama mfano wa watu wasiokuwa na hofu juu ya maisha yao. Wanaopata pesa yao kihalali kwa kusota, wakaitumia wapendavyo na kisha kuishi kwa amani wakilala nje bila kumhofia mtu yeyote na hata mdudu kama mbu naye asiwadhuru! Katika mfano huu alipenda kuhitimisha kwa kuniuliza, ni mwanasiasa gani (huu ulikinukiliwa enzi za Mkapa lakini bado una uhai) anaishi nyumba isiyo na geti kubwa, uzio wa umeme, walinzi wenye silaha, mbwa wakali  na Je, ana amani kuliko mimi au Rostamali?

Kulingana na kumbukumbu ya masimulizi mbalimbali, Dokta Kyaruzi ni miongoni mwa Watanganyika watatu wa kwanza kabisa kupata dalaja la Udaktari wa Binadamu. Na wa kwanza alitoka ukoo wa Kichifu pale Gera-Ishozi, Bukoba. Dokta Kyaruzi alikuwa miongoni mwa Maktaba zinazotembea. Ni mmoja wa watu waliomfahamu Mwl. J.K Nyerere fika tuliokuwa tumebaki nao. Kwa mara ya Kwanza Dokta walikutana na Mwl. Nyerere Tabora mwaka 1939 wakati Dokta akisoma St. Mary (Kwa sasa Milambo Sec. School) na Mwl. naye alikuwa akisoma Tabora School (Sasa Tabora Sec. School). Walibahatika kuwa wote tena katika masomo ya Elimu ya Juu huko Makerere-Uganda. Na kwa pamoja walishiriki siasa za ukombozi kupitia tawi la TAA Chuo Kikuu cha Makerere, Dokta akiwa kama Katibu wa Tawi. Waliporejea nchini kila moja alikwenda kwanza kutumikia fani aliyosomea huku akijipanga vema kushiriki siasa za ukombozi. Dokta Kyaruzi alikwenda kufanya kazi  Kingolwira wakati Mwl alikwenda kufundisha Tabora Boys. Baadaye hisia za ki-harakati ziliwarejesha Dar es Salaam na kuwakutanisha tena katika uongozi wa juu wa TAA huku Dokta Kyaruzi akikwea mpaka Uenyekiti wa chama mwaka 1949. Kama TAA ndiyo ilizaa TANU na TANU ikarithiwa na CCM basi utashangaa mbona Muasisi huyu hakuvuma na wala hukusikia habari zake kama usikiavyo habari za kina Sykes, Bibi Titi, n.k. Hili nakuachia uchunguze mwenyewe!  Miongoni mwa wanasiasa ambao Daktari amekufa akiwakumbuka kwa kumkumbuka au kuthamini harakati zake ni Prof. Mark James Mwandosya. Mwaka 2005 wakati Prof. Mwandosya akiwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi alifunga safari kwenda kumsalimu Daktari. Baada ya mazungumzo, Prof. Mwandosya alimwachia Daktari zawadi ya simu ya mkononi aina ya NOKIA. Ni jambo ambalo hakulisahau mpaka uhai unamtoka.

Baada ya uhuru, Mwalimu J.K Nyerere alimteua Dokta Kyaruzi kuwa Mwakilishi wa Kwanza wa Tanganyika huru kwenye Umoja wa Mataifa, NY-Marekani. Kutokana na uhaba wa wasomi baadaye Mwl alimuhitaji na hivyo Dokta Kyaruzi alirejea nchini na kuwa Msaidizi wa Mwl-Ikulu. Kulitokea uchonganishi kati ya wasaidizi wa Mwl uliojikita katika majungu ya madaraka. Na Mwl kwa kutolichunguza vema akafanya uamuzi wa kumrejesha Dokta Kyaruzi kufanya kazi kwenye taaluma yake. Hivyo Dokta Kyaruzi alipangiwa kuwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kazi ambayo aliripoti mara moja na kuitenda kwa moyo wake wote mpaka kustaafu utumishi wa umma. Aliporejea nyumbani Bukoba baada ya kustaafu alianzisha Zahanati iliyoangaliana uso kwa uso na duka la Nyegera Waitu. Kulingana na ugwiji aliokuwa nao katika masuala ya wanawake (Gynecology) huduma yake ilivuta watu kutoka sehemu mbalimbali za nchi na hata toka nchi jirani. Kipindi ziwa Rwelu (viktoria) likiwa ndo njia kuu ya usafiri kati ya Kagera na mikoa mingine, hakuna meli ingefika asubuhi bila kuwa na wagonjwa wanaokuja kupata huduma kwa Dokta Kyaruzi. Pamoja na huduma yake hii lakini pia aliendelea kutoa mchango wa Elimu, Uzoefu na Maarifa yake kupitia majukwaa mbalimbali. Lakini ushiriki wake katika harakati za kisisasa ulikomea katika uandishi wa makala kwenye gazeti la Rai.  Dokta amekuwa mjumbe na baadaye Mwenyekiti wa Bodi la Hospitali ya Mkoa wa Kagera kwa muda. Na katika kipindi chake mabadiliko makubwa katika miundombinu, rasilimali watu na huduma yaliweza kufanyika.

Hata katika umri wake wa mauti (miaka 91), Dokta ni mtu aliyeishi kwa kanuni na malengo. Siku yake iligawanywa kikanuni na haikubadilika iwe jua, umande ama mvua. Siku yake daima ilianza kwa kuhudhuria misa ya asubuhi. Baada ya misa hurudi nyumbani kupata kifungua kinywa na kujiandaa kwenda kazini. Saa saba alipata mlo wa mchana na kupumzika kwa saa na kisha kwenda kazini. Jioni alipenda kumpleleka mbwa wake ziwani na aliporejea alikaa bustanini kupata kikombe cha kahawa. Baada ya mazungumzo na mgeni ama kama muda wa sala ungefika  angali bado na wageni, basi angeomba udhuru na kwenda kusali na aliporejea alifikia mezani kwa mlo wa usiku. Mara baada ya chakula iwe cha mchana au usiku, Dokta asingeweza kuhimili nguvu ya usingizi hivyo kila baada ya mlo tendo lililofuatia lilikuwa ni kupumzika.

Dokta Kyaruzi alijaliwa uzao wa watoto wane (4). Miongoni mwao, wawili (Patrick na Christina) aliwapata kwenye ndoa ya kwanza na Mama wa Kiganda. Mama huyu walifahamiana wakati Dokta akisoma Makerere. Patrick alisomea urubani na Tina ni mtaalamu wa kushona mavazi aliyebokea. Mama Patrick alifariki kwa saratani zaidi ya miaka 35 iliyopita. Baada ya msiba huu Patrick na Tina ambao hawakuwa wakiishi Tanzania waligundua msongo uliompata Baba yao. Walibaini kuwa iwapo msongo usingetafutiwa njia mbadala mapema, basi ungempelekea Baba yao mauti mapema zaidi. Hivyo kwa pamoja wakamsihi Dokta aoe mwanamke mwingine. Huu ulikuwa ni wakati mgumu mwingine kwa Dokta Kyaruzi kuufanyia maamuzi. Baada ya kitambo Dokta Kyaruzi aliafiki kufunga ndoa na mke ambaye amepata kuzaa naye watoto wawili; wa kike (Adela-Ngonzi) na wa kiume ( Edween-Shubi)-Ni wiki chache tu Dokta Kyaruzi alikuwa amepata mjuu kupitia Adela ambaye kwa bahati mbaya sana mauti yamemkuta kabla ya kumtia machoni. Pia mjukuu wa Dokta aitwaye- John Patrick Kyaruzi, aishiye nje wiki jana tu ndo alikuwa amekata tiketi ya kuja Tanzania mwishoni wa mwezi kumsalimu Babu yake! Huzuni iliyoje?

Katika ndoa ya pili Dokta Kyaruzi hakudumu kabla ya kupata jaribu lingine kubwa. Wakati  ndoa inaanza kurejesha furaha na utulivu katika maisha yake, Patrick (mwanae mkubwa) aliyekuwa rubani wa ndege Marekani alipata ajali angani na ndege kuteketea.  Kilichoshuhudiwa na kuzikwa ni majivu! Ukifuatilia vema maisha ya familia ya Dokta Kyaruzi utaduwaha kubaini mlolongo wa ajali za ndege na hasara zake katika mali na watu wa familia.

Katika maisha yake yote pamoja na utitiri wa fursa alizokuwa nazo, Dokta Kyaruzi alimiliki nyumba mbili tu; moja Kyaka-Mutukula na nyingine Miembeni-uwanja wa ndege, Bukoba. Nyumba ya Kyaka ilitunguliwa na ndege wakati wa vita ya Kagera na ile ya miembeni iliunguzwa upande kwenye ile ajali ya ndege ya Jeshi ya mwaka 1997. Wale mtakaokumbuka, pamoja na nyumba kuungua upande, Dokta Kyaruzi alipoteza magari yake mawili (Toyota Stout na Jeep) papo hapo. Pia vifaa vya Zahanati yake ambayo alikuwa ameihamishia nyumbani viliharibika na kupelekea huduma kufungwa. Hizi ajali na matokeo yake huniumiza sana hadi leo. Hata mara zote Dokta Kyaruzi alipokuwa akizirejea katika masimulizi, zimekuwa zikiniacha na  simanzi kubwa. Kiufupi, HAKUNA FIDIA YOYOTE ALIYOPEWA Dokta Kyaruzi katika ajali hizi! Si kwa sababu yoyote ile ya msingi bali ni kutokana na ukiritimba na rushwa ambazo yeye hakuwa tayari kuafikiana nazo. Katika upanuzi wa uwanja wa ndege uliofanyika hivi karibuni, Dokta Kyaruzi alitakiwa kubomoa na kuondoka toka nyumba hii ya Miembeni. Kwa tabia yake ya kupenda kutenda na kutendewa haki alimanusura anyimwe hata kile kiduchu cha fidia aliyopewa. Mpaka pale Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi alipoingilia kati.

Ndugu na Jamaa tunamlilia mpendwa wetu Dokta Kyaruzi. Na kwa tabia ninahakika na viongozi wa Serikali-Kitaifa nao sasa watanakshi salamu na hotuba zao. Binafsi hisia zangu zinahama haraka kutoka kwenye huzuni na kujawa na furaha na amani ya moyo. Ni kwa kuwa imani yangu inanituma kuamini kuwa Dokta Kyaruzi hakufa bali ametwaliwa kwenye makazi ya kudumu akafurahie milele kifuani mwa Ibrahim  baada ya kuyashinda majaribu makuu ya ulimwengu huu. Siku zote nimeyatathmini maisha ya Dokta Kyaruzi kwa kuyamithilisha na miasha ya Ayubu mtumishi wa Mungu. Naamini hata katika kulifanya simulizi langu kuwa fupi kadri niwezavyo bado umeweza kung’amua mateso na majaribu aliyopitia Dokta Vedasto Kyaruzi.

No comments:

Post a Comment