Sunday, May 13, 2012

BENKI KUU: HAZINA YA TAIFA IMEKAUKA?

Zitto Kabwe, Mb.

Benki Kuu ya Taifa lolote ndio taasisi pekee yenye takwimu zote nyeti na za uhakika zinazohusu uchumi wa Taifa hilo. Katika tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania eneo la Machapisho kuna Taarifa nyeti sana mbili, Mapitio ya Uchumi ya Mwezi (Monthly Economic Review) inayotoka kila Mwezi katika Mwaka na Mapitio ya Uchumi ya Robo Mwaka (Quarterly Economic Bulletin). Taarifa hizi hutoa taarifa kuhusu masuala yote muhimu yanayohusu Uchumi wa Jamhuri ya Muungano na Uchumi wa Zanzibar ikiwemo taarifa za Mfumuko wa Bei, Mapato na Matumizi ya Serikali, Mwenendo wa Biashara ya

Kimataifa na Deni la Taifa.

Ukienda kwenye tovuti ya Benki Kuu leo utakuta Taarifa hizi. Lakini Taarifa hizi zimeishia Desemba mwaka 2011 zikitaarifu masuala ya Uchumi ya Mwezi Novemba na robo ya mwaka inayoishia Desemba. Ukitaka kujua Bajeti ya Serikali na mwenendo wake hutapata taarifa za sasa bali za Mwezi Novemba mwaka 2011, miezi sita nyuma. Huu sio utendaji uliotukuka. Hii ni kuficha taarifa kwa wananchi. Taarifa zinafichwa ili iwe nini? Nani anafaidika na kufichwa kwa taarifa muhimu kama hizi?

Kuna tetesi kwamba Hazina ya Taifa (Hifadhi ya Fedha za kigeni – foreign reserve) inakauka, kwamba tuna hifadhi ya kuagiza bidhaa nje kwa mwezi mmoja tu. Niliposikia tetesi hizi sikuamini. Nilipoenda katika tovuti ya Benki Kuu ili kuweza kuwa na habari rasmi (authoritative) nimekuta takwimu za Novemba 2011.

Takwimu ya Mfumuko wa Bei iliyoko kwenye tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania ni ya mwezi Novemba mwaka 2011!

Ukitaka kujua mwenendo wa Bajeti ya Serikali kama makusanyo ya Kodi na Matumizi utapata Taarifa ya Mwezi Novemba mwaka 2011.

Ukitaka kujua manunuzi ya Mafuta (fuel imports) kwa miezi 3 ya mwanzo ya mwaka 2012 ili kuweza kuona namna Umeme wa dharura umeathiri urari wetu wa Biashara ya Nje hupati taarifa hiyo katika tovuti ya Benki Kuu.

Taarifa zinafichwa.

Ndio. Zinafichwa tena makusudi maana taarifa hizi zipo Benki Kuu. Huu ni uzembe maana Nchi inawalipa wafanyakazi wa Benki Kuu mishahara minono ili wafanye kazi hizi. Benki Kuu pia imetoa zabuni kwa Kampuni Binafsi kuchapisha Taarifa hizi. Kama Taarifa hazitoki kwa wakati ni wizi. Wizi ambao haupaswi kufumbiwa macho.

Benki Kuu ya Tanzania ipo miezi Sita nyuma. Aibu kubwa sana.

Wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano akihakikishia mataifa duniani kuhusu uwazi Serikalini (#OGP), Taasisi kubwa kama Benki Kuu inaficha Taarifa ambazo ni nyeti kwa wananchi na muhimu kwa wafuatiliaji wa sera za Serikali. Rais wa nchi anaongea Buluu, Gavana wa Benki Kuu anasimamia Kijani!

Inaudhi na kukera sana kwenda kwenye tovuti ya Benki Kuu na kukuta taarifa za miezi Sita iliyopita. Benki Kuu hamstahili kuitwa Benki Kuu, labda benki kuu kuu. Rekebisheni jambo hili haraka sana maana kuficha taarifa kwa Umma ni ufisadi. Haki ya kupata taarifa ni haki ya msingi katika Katiba yetu.  Hatutaki kushtukizwa na kuambiwa Hazina ya Taifa imekauka.

Prof. Ndulu hakikisha Taarifa ya Mapitio ya Uchumi wa kila Mwezi imewekwa kwenye tovuti kwa muda mwafaka. Ifikapo mwisho wa Wiki inayoanzia Jumatatu Mei 14, tovuti ya Benki Kuu iwe na Taarifa za miezi yote (Desemba, Januari, Februari, Machi na Aprili). Taarifa hizi ni muhimu ili nasi tutekeleze majukumu yetu ya Kikatiba kama Wabunge, Mawaziri vivuli na Wananchi wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment