Mbunge wa Maswa Magharibi (CHADEMA) John Shibuda akisalimiana na Rais Kikwete.
BAVICHA imepokea kwa mshituko mkubwa kauli ya ndugu Shibuda kuwa
yeye atagombea Urais na Meneja wake wa Kampeni atakuwa Mwenyekiti wa CCM
ndugu Jakaya Kikwete, na alitoa kauli hiyo kwenye kikao cha NEC ya CCM.
MAMBO YAFUATAYO YEMETUSHTUA;
1. Katoa Kauli hiyo kwenye kikao cha NEC ya CCM
2. Meneja wa kampeni zake amemtangaza kuwa ni Mwenyekiti wa CCM taifa Jakaya Kikwete
3. Amesema kuwa hakuna chama kingine chenye uwezo wa kuiongoza nchi kwa sasa.
4. Alitoa tamko hilo kwa niaba ya APRM .
Mambo hayo manne ndio yametushtua na kutufedhehesha sana sisi
vijana wa CHADEMA na ndio maana tumelazimika kutoa kauli kuhusiana na
suala hili , na kauli yetu ni kama ifuatavyo;
1. Kamwe BAVICHA hatutaruhusu mgombea Urais wa CHADEMA meneja wake
wa kampeni awe ni Mwenyekiti wa CCM hata siku moja kwani tunao watu wa
kutosha na wenye uwezo wa kutosha kuifanya kazi hiyo na hatuhitaji
msaada huo .
2. Kamwe hatutaruhusu mgombea urais wa CHADEMA awe anatangaza
nia kwenye vikiao vya CCM kwani hawana mamlaka ya kumteua mgombea wa
CHADEMA na kama Shibuda alikuwa halijui hilo anapaswa kulifahamu kuanzia
sasa kuwa vijana wa CHADEMA hatuchaguliwi mgombea na NEC ya CCM kwani
CHADEMA kuna vikao na taratibu zetu za kuteua wagombea.
3. Kusema kuwa hakuna chama kingine chenye uwezo wa kuongoza
nchi ni kutudhalilisha sisi vijana wa CHADEMA na watanzania wote ambao
leo wanaiona CHADEMA kama tumaini pekee la kuwakomboa, kauli hii
tunaamini kama vijana wa CHADEMA kuwa mamlaka za nidhamu hazitakaa kimya
na kuiachia kauli ya namna hii iachwe bila kutakiwa maelezo ya kina ,
tutaitisha kikao cha BARAZA na tutaijadili kauli hii na kuwasilisha
mapendekezo yetu kwenye vikao halali vya chama .
4. Tunapenda kumwambia kuwa kama anaona kuwa yeye haendani na
utamaduni wa chama chetu na anakiona kuwa hakina uwezo wa kuongoza dola
anafanya nini kwenye chama ambacho anona kuwa hakiwezi kuongoza dola?
Kwanini atafute urais kwenye chama ambacho anaona hakiwezi kuongoza dola
? anawatania watanzania? Ni heri akaenda kwenye hicho ambacho anaamini
kuwa kinaweza kuongoza dola , kwani lengo la chama chochote kile ni
kuchukua dola na sio vinginevyo.
5. Mwisho tunapenda kuwahakikishia vijana wote wa Tanzania na
wananchi kwa ujumla kuwa tayari CHADEMA kimejiandaa kikamilifu kuongoza
dola na wasiwe na hofu na maneno yaliyotamkwa na Mbunge huyu .
6. Natoa wito kwa Vijana wenzangu wote wa CHADEMA kuwa sasa
tujiandae kikamilifu katika kukabiliana na mtu yeyote yule ambaye
ataonekana kuwa kikwazo kwa chama chetu na wananchi kwa ujumla wake
katika kuelekea kuchukua dola 2015 .
Nawatakia kila la kheri katika ujenzi wa chama na tuendeleze operesheni ya ‘Vua Gamba, Vaa Gwanda’ popote pale tulipo nchini.
Imetolewa leo Dar es Salaam,
Mei 16, 2012 na;
John Heche
Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa.
No comments:
Post a Comment