Wednesday, May 9, 2012

Obama aunga mkono ndoa za jinsia moja

Rais Obama ameunga mkono ndoa za jinsia moja kama hii
Rais Barack Obama amesema kwamba watu wa jinsia moja wawe na haki ya kuoana.
Bwana Obama amesema daima amekuwa mgumu kukubali kwamba wanaume na wanawake wenye uhusiano wa mapenzi ya jinsia moja nchini Marekani watendewe haki na jamii kwa kutambua uhusiano huo, lakini amekuwa akipitia kile anachokiita mabadiliko ya kimtazamo kuhusu suala la ndoa za jinsia moja.
Kwa kauli hii Obama anakuwa rais wa kwanza wa Marekani kuunga mkono ndoa za jinsia moja, suala ambalo limeleta mgawanyiko miongoni mwa raia wa Marekani. Kumekuwa na maoni tofauti miongoni mwa Wamarekani kuhusu kuunga mkono ndoa za aina hii.
Rais Obama anasema amejadili suala hilo na familia, marafiki na majirani kwa muda mrefu na kutilia maanani wafanyakazi wenzake na askari ambao wamejikita katika uhusiano wa mapenzi ya jinsia moja.
Hatimaye amekuja na hitimisho kwamba ndoa zilizozoeleka hazikidhi matarajio ya wote.
Mpinzani wake katika uchaguzi wa rais wa mwaka huu, Mitt Romney, wa chama cha Republican amesema bado anabakia kupinga ndoa za watu wa jinsia moja.
Amesema wakati akiunga mkono ndoa ambazo hazijatambuliwa kisheria, kwa maoni yake, suala la ndoa za kawaida ni jambo lingine tofauti na hizo ndoa za jinsia moja.
Kauli ya Bwana Obama, imekuja siku moja baada ya jimbo la North Carolina kupitisha mabadiliko ya katiba ya jimbo hilo, yanayofafanua kuwa ndoa ni muungano tu kati ya mwanaume na mwanamke.

No comments:

Post a Comment