Tuesday, May 8, 2012

Waasi washindwa DRC

Wanajeshi wa DRC

Jeshi nchini DRC linasema limedhibiti eneo zima la Masisi kutoka kwa waasi watiifu kwa kiongozi wa waasi Bosco Ntaganda.
Jeshi limetangaza kusitisha mapigano na kuwapa waasi hadi siku ya Jumatano kujisalimisha.
Maelfu ya watu wametoroka makwao katika eneo hilo baada ya wiki nyingi za mapigano.
Generali Ntaganda, ambaye anajulikana kwa jina lengine kama "The Terminator", anatakiwa na mahakama ya kimataifa ya ICC kwa makosa ya jinai.
Mahakama hiyo inamtuhumu Ntaganda kwa kuandikisha watoto kama wanajeshi katika kundi moja lililokuwa tiifu kwa Thomas Lubanga, ambaye mwezi Machi alikuwa mtu wa kwanza kupatikana na hatia ya uhalifu wa kivita katika mahakama ya ICC.
Wanajeshi wake, waliondoka katika jeshi la serikali mwezi jana na maafisa wakuu nchini Congo wanasema kuwa wanataka ahukumiwe nchini Congo badala ya kupelekwa Hague.
Mamia ya wanajeshi watiifu kwa Ntaganda, waliteka miji miwili huko Masisi, karibu na mkoa wa Kivu kaskazini na Goma, lakini Luteni generali wa jeshi,Didier Etumba Longila alisema kuwa eneo hilo zima limedhibitiwa na jeshi la serikali.
Hata hivyo msemaji wa jeshi Luteni kanali Sylvain Ekenge, alisema kuwa afisaa mmoja mkuu wa jeshi alijiunga na waasi hao mnamo siku ya Ijumaa.

No comments:

Post a Comment