Wednesday, May 9, 2012

Shehena kubwa ya silaha yanaswa DRC

Jenerali Ntaganda: Silaha zimenaswa kwa shamba lake
Shehena kubwa ya silaha imenaswa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika shamba linalomilikiwa na mbabe wa kivita wa zamani Jenerali Bosco Ntaganda.
Kwa mujibu wa jeshi, silaha nyingine zimenaswa katika maeneo mengine mawili katika Mkoa wa Kivu ya Kaskazini, eneo ambalo lilikumbwa na mapigano kati ya wanajeshi na waasi. Inadaiwa silaha hizo zilikuwa za wapiganaji watiifu kwa Jenerali muasi Bosco Ntaganda.
Tukio hili linajiri siku moja kabla ya kukamilika kwa muda waliopewa waasi watiifu kwa Ntaganda kujisalimisha au wakabiliwe kijeshi.
Kanali Innocent Gahizi ambaye ni kamanda mkuu wa operesheni katika Mkoa wa Kivu ya Kaskazini ameiambia BBC, kuwa malori matatu yaliyosheheni bunduki za rashasha na grunedi yamenaswa na jeshi katika maeneo ya Singi, Mushake na Kirorirwe.
Gahizi ameongeza kuwa jeshi limetwaa uthibiti wa maeneo yote mashariki mwa Masisi na limetangaza mpango wa kusitisha mashambulio ili kuwapa waasi hao muda wa kujisalimisha kabla usiku wa manane.
Jenerali Ntaganda anayejulikana kama Terminata katika jina la utani, anasakwa na mahakama ya ICC kwa tuhumu za uhalifu wa kivita.
Anatuhumiwa kuwasajili watoto kuwa wapiganaji wa kundi la waasi la Thomas Lubanga, ambaye alikuwa mtu wa kwanza kuhukumiwa na mahakama hiyo ya ICC mwezi Machi mwaka huu.
Jenerali Ntaganda ambaye amehusika na mashambulio kadhaa nchini humo kwa miaka mingi, amekanusha madai ya kuchochea uasi ndani ya jeshi, akitumia wanachama wa zamani wa kundi la waasi wa CNDP.

No comments:

Post a Comment